OFISA Habari wa Klabu ya Yanga, Jerry Muro, amesema ameiombea klabu
yake hiyo kwa Nabii maarufu nchini Nigeria, T.B Joshua, alipokwenda
nchini humo kwa ajili ya shughuli zake binafsi.
Muro ni mmoja wa Watanzania walioshiriki misa ya Jumapili katika
kanisa la nabii huyo maarufu Afrika, ambaye anasifika kwa utabiri wa
kweli.
Umaarufu wa TB Joshua ulishika kasi nchini mwaka jana katika Uchaguzi
Mkuu uliofanyika Oktoba, baada ya waliokua wagombea wa nafasi ya urais,
Rais wa sasa, John Magufuli (CCM) na Edward Lowassa (Ukawa) kufika
Nigeria kabla ya uchaguzi huo kwa ajili ya maombi.
Mbali na kuwaombea wagombea hao, T.B Joshua siku moja kabla ya
kuapishwa Rais wa Awamu ya Tano, Magufuli, Novemba 4 alifika nchini na
kupokelewa na Rais huyo ambapo baadaye alikutana Ikulu na Rais mstaafu
Jakaya Kikwete.
Baada ya hapo T.B Joshua alikutana na Lowassa ambapo baadaye alifanya
misa ya pamoja na familia yake kabla ya kuondoka kurudi Nigeria.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Muro alisema alienda kwa Nabii huyo
kwa ajili ya mambo yake binafsi, pia alishiriki ibada iliyofanyika
Jumapili iliyopita katika kanisa lake.
“Ilikua Jumapili muhimu kwangu, nilishiriki ibada mbali ya kujiombea
na familia yangu niliiombea klabu yangu pendwa ili iweze kufanya vizuri
katika michuano ya Ligi Kuu na ile ya kimataifa ikiwemo kuchukua mataji
hayo.
“Niliondoka nchini Jumatano Aprili 20 na nimerudi jana (juzi) usiku,
kwakweli najisikia ni mtu mwenye amani na sasa nipo Mwanza nimeambatana
na timu hapa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Toto,” alisema.
Muro alisema furaha yake ni kuona Yanga inapata mafanikio.
Wakati huo huo, wapinzani wa Yanga katika hatua ya 16 bora ya
michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Sagrada Esperanca, juzi
walikiona cha moto kwenye Ligi Kuu ya nchini Angola baada ya kufungwa
mabao 2-0 dhidi ya Interclude.
Kipigo hicho kilitibua maandalizi ya Waangola hao kabla ya kuikabili
Yanga Mei 6, mwaka huu kwani kimewafanya washuke kutoka nafasi ya nne
hadi ya saba kwa kufikisha pointi 13 wakiwa wameshuka dimbani mara tisa.
0 comments:
Post a Comment