
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amefichua kuwa vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi na vigogo wa serikali ndiyo sababu ya kuchukiwa kwa serikali ya chama tawala.
Kutokana
na hali hiyo, amewaomba wananchi wampigie kura nyingi za ndiyo ifikapo
siku ya uchaguzi, Oktoba 25, mwaka huu ili awachukulie hatua na
kukomesha hali hiyo.
Akizungumza
katika mkutano wake wa kampeni mjini Hanang, mkoa wa Manyara jana, Dk.
Magufuli alifafanua kuwa yeye ni tingatinga na Watanzania wakimpigia
kura nyingi na kumuingiza Ikulu atawaonyesha namna atakavyosafisha
mafisadi serikalini na mwishowe kuwezesha maisha bora kwa kila mmoja.
Dk.
Magufuli alisisitiza kuwa akiingia Ikulu, kamwe hatakuwa na msamaha
dhidi ya mafisadi na wala rushwa kwani mara zote wamekuwa chanzo cha
kukwamisha huduma za jamii zinazotolewa na serikali na kusababisha
wananchi waichukie serikali yao.
Alirudia
kauli yake anayoitoa karibu katika kila mkutano kuwa ataanzisha
mahakama ya mafisadi ili kuhakikisha analinda rasilimali za umma ambazo
zimekuwa zikiibwa na watu wachache.
Alisema
anatambua kuwa hivi sasa Watanzania wamechoshwa na maisha duni, hivyo
wanahitaji kuwa na rais kama yeye ambaye atasimamia mabadiliko ya kweli
ili kila Mtanzania afaidi maisha bora .
“Niombeeni
ili nikiingia Ikulu nisiwe na kiburi... nataka niwatumikie Watanzania
wote bila kujali vyama vyenu, maana mmeteseka sana na shida
zilizosababishwa na mafisadi. Vitu vimepanda bei kwa sababu ya ufisadi.
Nataka kukomesha yote hayo,” alisema.
Aliongeza
kuwa anatambua mikakati ya mafisadi ambao wamejipanga kutoa rushwa ili
kuwarubuni wananchi wawachague kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Fedha
chukueni, lakini kura ni kwa Dk. Magufuli tu. Zile fedha watakazogawa
ni zenu. Walizichukua kwa wizi walipokuwa madarakani, zichukueni, lakini
tarehe 25 wataisoma namba,” alisema.
0 comments:
Post a Comment