Thursday, October 1, 2015

Hakuna Ray wa ‘Kutisha’ Bila Marehemu Kanumba...Wema, Aunt Ezekiel, Swebe na JB wafunguka

 
Hatimaye muigizaji Vicent Kigosi wiki hii amekiri kuwa msisimko na ushindani wa kutoa, kuigiza filamu kali uliokuwepo wakati marehemu Steven Kanumba akiwa hai, haupo tena.
Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, huku mashabiki na wadau mbalimbali wa filamu wakiliona hilo, hasa kuitokana na kutokuwepo kwa filamu za kuvutia, kushindana kupiga pamba kali, magari ya kifahari, safari za nje ya nchi.

Ray alikaa kimya muda mrefu kulizungumzia hili hatimae amekubali kuwa ni kweli hakuna vitu vyote hivyo baada ya aliyekuwa mshindani wake mkuu kufariki kwa maana hiyo “ Hakuna Rey Bila Kanumba”.

Baadhi ya wasanii kama Aunty Ezekiel , Rose Ndauka, Mayasa Mrisho, Batuli, wamekiri kitambo na bdo wanaeleza upungufu wa tasnia hiyo baada ya kifo cha Kanumba.

Ushindani wao uliamsha hisia kwa mashabiki wadau

Waigizaji hawa walianza wote kwenye kampuni ya filamu iitwayo Mtitu Games 1st Quality , mwaka 200-2007 walicheza filamu nyingi na hata kufanikiwa kuingiza filamu katika soko la kununua CD badala ya kurushwa kwa vipande kwenye luninga.

Filamu iliyokuwa kali wakati huo na iliyowatambulisha ilijulikana kwa jina la Johari na ndiyo iliyozaa jina la mwigizaji Blandina Chagula kuitwa Johari, hapo bado walikuwa kwenye kundi maarufu la Kaole Sanaa Groupe, baada ya hapo waliigiza filamu kama Dangerous Desire, Oprah, Sikitiko Langu, Penina.

Walipojiunga pamoja kwenye kampuni ya Mtitu Games 1st Quality, Ray aliona mbali akaamua kuondoka na kujipanga kivyake huku, Kanumba akibaki na kusoma upepo ambapo alizidi kung’aa pia kwani kwa msaada wa Mtitu aliweza kuigiza filamu kama “Dar to Lagos”, “Cross My Sin” ambazo aliigiza na waigizaji wa Nigeria akiwamo Mercy Johnson.

Ray alipotoka alianzisha kampuni yake ya RJ , akishirikiana na Johari, Kanumba nae akafuatia na kuanzisha yak wake aliyoiita Kanumba Great Films

Marehemu Kanumba ndiyo alikuwa wa kwanza kuibua ushindani kati yao uliopelekea kushindana kwenye mambo mengi na kuwagawa mashabiki kama ingekuwa leo ingekuwa timu Ray na timu Kanumba. Mwaka 2010, Kanumba alinunua gari aina ya Toyota hiace la kufanyia biashara akaliandika Kanumba The Great, kabla ya Ray kununua kama hilo na kuliandika Ray The Greatest.



Kama hiyo haitoshi walishindana pia kununua gari za kutembelea ambapo kama nilivyosema waliwapa shida mashabiki wao Ray alinunua Toyota Land Cruiser V8 na kujinasibu lina thamani ya 60 milioni na Kanumba akanunua Toyota Lexus na kujinasibu kuwa la sh 78 milioni. Hapa napo timu za Ray na Kanumba zilikuwa nyingi kupita maelezo kila upande ukisema wake ndiyo mkali.

Ukitaka kufahamu ushindani wao uliohamia kwa mashabiki wao ulikuwa na faida ni pale mmoja kati ya waigizaji hao alipotangaza kuja kwa filamu mpya, ilikuwa heka heka kila timu ikiwa na hamu ya kuona filamu yao mpya, hivyo kuwa gumzo kama sasa Diamond anapoachia wimbo.

Mazugumzo hayo kuhusu kuzichambua kazi zao yalizifanya ziwe na mvuto hata kununuliwa na kuwapo kwa ushindani wa kweli wa kufanya kazi nzuri, kwani kama walivyoanza hakuna aliyekubali kushindwa na mashabiki walikuwa ndiyo majaji wa kazi hizo.

Kanumba akazidi kupanda chati baada ya kuanza safari za nje ya nchi akitafuta kufanya kazi na wasanii wakubwa wa Kimataifa kama Nancy Okeke , Nkiru Silvanus, Mercy Johnson na Bimbo Akintola.

Ray nae alijitahidi ingawa hakufika mbali katika uigizaji, lakini kwenye vifaa vya kazi Kanumba alikwenda kununua Marekani, Ray akaenda Singapore, hii ilizidi kuwapa nguvu mashabiki zao.

Hivi sasa Ray hatajwi tena, alijitahidi Jackob Steven JB , lakini anahitaji kuongeza nguvu kutunga hadithi za kuvutia, kwani Kanumba licha ya kushindana na Ray pia alikuwa anatunga hadithi nzuri za filamu zilizokuwa na mvuto.

Wasanii waungana na Ray tena

Swebe Santana
Tangu kuondoka Kanumba hakuna soko la filamu tena, hakuna hadithi za filamu mpya iliyotoka mitaani, kimekuwa kitu cha kawaida watu wanashabikia mipira na habari mpya magazetini siyo filamu.

Havitafutwi vipaji vya kuigiza kama enzi zake sasa ni majina na sura, mzuri, anayejulikana anaigiza hata kama hajui, pengo lake litabaki kuwepo hata iweje, hata hao waliovuma wakati wake hawana hali nzuri kisanii watafute kazi ya kufanya.

Aunty Ezekiel
Hakuna wa kubisha hali ipo hivyo, hakuna ushindani wa kuigiza , watu wanaangalia fedha , hawaangalii maudhui na watayatendeaje haki, inaweza kutoka filamu uliyoigiza na usisikie ikizungumziwa.

Kwenye muziki kuna watu wana nguvu, lakini kwenye filamu hivi sasa hakuna baada ya kuondoka Kanumba tasnia basi, inahitaji nguvu kubwa kuiinua kwani kadri siku zinavyozidi hali inakuwa tete.

Wema Sepetu
Kuigiza suala moja na kupeleka tasnia mbele suala lingine, Kanumba alimudu vyote, alifanya vizuri ndani na alijipambanua Kimataifa na kufanya sanaa ya filamu Bongo itambulike nje ya Bongo.

Hilo limekwamia hapo na sifahamu kama tutaweza kujikongoja tena, wapo tunaojaribu lakini bado tunahitaji kuungwa mkono sana kuhakikisha tunafanya kama alivyofanya yeye.

Ushindani hauridhishi, hakuna umoja wa kweli, mmeguko unaweza kuwa chanzo cha hayo, Inshallah tukijipanga tunaweza kujikwamua ingawa tunahitaji kutumia nguvu nyingi kwa sababu tumekubali kurudi nyuma.

JB
Alifanya kwa wakati wake na sisi tunaendeleza alipoachia kila kitu hakiwezi kuwa sawa kwa sababu wakati ule ndiyo alikuwa anaanza, hivyo labda angekuwepo tungefika mbali.

Lakini bado tunafanya juhudi kuhakikisha tunafika mbali, kwani bado watu wanaigiza, kazi nzuri, na vipaji vipya kila siku vinazaliwa, muhimu ni kuhakikisha tasnia inasonga.

Baadhi ya filamu za kuvutia alizowahi kuigiza marehemu Steven Kanumba

“Uncle JJ”, “Young Billionaire”, “Big Daddy”, “Magic House”, “Moses”, “Village Pastor”, “Crazzy Love”, “Devil Kingdom”, “Red Valentine” na “The Lost Twins”.

Chanzo: Gazeti La Mwananchi
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger