Friday, May 13, 2016

Wabunge 53 Chadema na CUF Wajitoa TWPG Baada ya Kutoombwa Radhi na Mbunge wa CCM Aliyedai Wamepata Ubunge Kwa Kufanya Mapenzi

WABUNGE wanawake 53 wa kambi ya upinzani kutoka vyama vya CUF na Chadema wamejitoa kwenye Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG) baada ya kutoombwa radhi na Mbunge la Ulanga, Godluck Mlinga (CCM) aliyesema wabunge hao kutoka Chadema walipata ubunge kwa njia ya mapenzi.

Mlinga alisema wabunge wanawake ndani ya Chadema, walipata nafasi hiyo baada ya kuwa ‘baby’ wa watu. Alitoa kauli hiyo wakati anachangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni Mei 5 mwaka huu.

Sambamba na hilo, alisema wabunge wa ndani ya chama hicho wamo pia wenye uhusiano wa jinsia moja. Hata hivyo hakuwataja kwa majina wabunge hao.

“Kila mwanamke ndani ya chadema kaingia ubunge kwa sifa yake lakini sifa kubwa ni lazima uwe baby (mpenzi) wa mtu. Ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja,” alisema Mlinga. 

Katika barua yao ya kujitoa jana iliyosainiwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa niaba ya wabunge wenzake wa kambi ya upinzani na nakala kupewa Spika, Job Ndugai, ilieleza kuwa kauli ya Mlinga inadhalilisha wabunge hao, utu na heshima ya mwanamke.

“Licha ya juhudi zilizofanywa na wabunge wa upinzani za kutaka mbunge husika(Mlinga) afute kauli yake , juhudi hizo hazikuzaa matunda kutokana na Naibu Spika(Tulia Ackson) kupuuza miongozo iliyokuwa ikiombwa.

"Na kikubwa alichokifanya baada ya mbunge (Mlinga) kumaliza kutukana ni kuwataka watu wa hansard wafute kwenye kumbukumbu za Bunge, kitu ambacho ni kinyume na matakwa ya Kanuni za Bunge,”alisema Mdee kwenye barua hiyo iliyosainiwa na wabunge wa CUF 10 na wa Chadema 43.

Alisema wabunge wa upinzani walisononeshwa zaidi na wabunge wenzao wanawake wa CCM, wakiongozwa na aliyekuwa Katibu wa TWPG, Angela Kairuki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge,Vijana, Ulemavu na Ajira, Jenista Mhagama kushangilia udhalilishaji huo.

“Ukimya wenu kwenye matukio haya na ushiriki wenu katika kushangilia wakati wanawake wanadhalilishwa inatufanya tuhoji mantiki ya uwepo wetu katika umoja huu ambao tunaambiwa malengo na dhamira yake ni kutuunganisha wanawake katika kumkomboa, kumpigania na kulinda haki na utu wa mwanamke,” alisema Mdee.

Wabunge hawa wanajitoa licha ya baada ya tukio hilo, umoja huo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Margaret Sitta kulaani na kueleza kutokubaliana na tabia ya baadhi ya wabunge ya kutumia lugha za matusi, kejeli ,dharau na udhalilishaji wa wabunge wanawake kutoka Chadema kuwa wamepata nafasi hiyo kwa njia ya kuwa ‘baby’ wa mtu.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger