Spika
wa Bunge, Job Ndugai, ametaja sababu zinazochochea wabunge kujiingiza
kwenye vitendo vya rushwa, ni presha kutoka kwa wananchi inayotokana na
kutakiwa kuchangia masuala mbalimbali katika majimbo yao.
Spika
huyo pia amewatangazia rasmi wabunge kuwa Ofisi ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria utakaotenganisha uongozi na biashara.
Aliyasema
hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Chama cha Wabunge
wanaopambana na Rushwa (APNAC), mjini Dodoma. Aliwataka wabunge hao
kujiepusha na vitendo vya rushwa licha ya kuwa na maslahi madogo.
Pia aliwataka wajiandae na sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa katika bunge hilo wabunge wengi pia ni wafanyabiashara.
Presha za rushwa
Alitaja
sababu za wabunge wa Tanzania kujiingiza kwenye rushwa ni presha za
wananchi wao kuwataka wachangie kila inapotokea msiba, sherehe,
madawati, madarasa, barabara hadi ada.
Alisema
kutokana na kipato kidogo cha fedha, wabunge wengi hutafuta mbinu
mbadala za kupata fedha kumudu gharama hizo. Mishahara ya wabunge na
marupurupu yake kwa mwezi yanakadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 11
kwa mwezi.
Sababu
nyingine ni mikopo yenye riba kubwa ambayo wabunge wengi wameichukua
ikiwa ni pamoja na maslahi madogo wanayopata wabunge hao.
“Kutokana
na hali hii wakati mwingine humfanya kiongozi ahangaike kutafuta fedha
na ndipo wengine hujiingiza katika vitendo hivi vya rushwa.
"Nawatahadharisha ninyi kama wabunge mnao wajibu wa kudhibiti rushwa na kuwa mfano katika jamii,” alisema.
Spika alilia maslahi
Alisema
katika eneo la maslahi, ofisi ya Bunge inatambua kuwa bado maslahi
wanayopata wabunge hao ikilinganishwa na kazi wanayofanya ni madogo
hivyo, wanaendelea kuangalia namna ya kuyaboresha.
Ndugai
alisema wabunge wa Tanzania wana wajibu na jukumu kubwa la kudhibiti
rushwa kwa kutunga sheria zinazopaswa kutumika katika kuunga mkono au
kuleta miswada itakayosaidia kutokomeza rushwa. Alisema pia moja ya kazi
ya wabunge ni kushauri na kusimamia Serikali.
Alisema ni vyema pale ambapo kuna viashiria vya rushwa wakatoa ushauri huo bila kukubali kushawishiwa kwa rushwa.
“Vilevile
katika kupitisha bajeti za serikali, hapana budi kuhakikisha vyombo
vinavyohusika na mapambano dhidi ya rushwa vimetengewa fedha za
kutosha,” alisema.
Aliwaasa
wabunge kujiepusha na vishawishi vya rushwa kwa kuwa nafasi waliyonayo
ni nyeti. Alisema pia kutokana na mwenendo wa umakini wa Serikali ya
Awamu ya Tano, inawezekana wakawepo watu wanaoona umakini huo kama
maslahi yao na kutumia njia pekee ya kuwarubuni wabunge.
“Nawaasa
msishawishike,” alisisitiza. Alisema kwa mujibu wa Jumuiya ya Vyama vya
Wabunge Wanaopambana na Rushwa Afrika (GOPAC), takribani dola za
Marekani bilioni 50 hutoroshwa Afrika kutokana na rushwa. “Hizi ni fedha nyingi sana za walalahoi zinazotumika kwa maslahi ya wachache,” alisema.
Pia
amehamasisha wabunge hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kile
alichosema, katika awamu hii ya serikali ya awamu ya tano, yeyote
atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo lazima aingie matatani.
Sheria ya maadili
“Muda si mrefu nitawaalika waje watoe semina kwenu kuhusu undani wa sheria hiyo ili wote muielewe vyema.
"Nawashauri muisome vizuri sheria hii ikija kwa sababu wengi wetu pamoja na ubunge tunafanya biashara ili tujiendeshe vizuri,” alisisitiza Ndugai.
Alisema
sheria hiyo ikipitishwa, haitakuwa ya kwanza Tanzania kuitekeleza kwani
nchi nyingi duniani zimekuwa na mfumo unaotenganisha viongozi wake na
biashara.
“Wenzetu
ni kawaida ukiingia kwenye siasa unakabidhi biashara yako mpaka pale
utakapomaliza uongozi wako ndio unaruhusiwa kuendelea, naomba mjiandae
kuipokea sheria hii, ni sheria nzuri na ina malengo mazuri,” alisema.
Akizungumzia rushwa, alisema kila bunge lina sababu zake za wabunge kujiingiza katika vitendo vya rushwa .
APNAC yapongeza kupunguza rushwa
Akiwasilisha
mada ya kuhusu tathmini ya shughuli za APNAC katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Davis Mwamfupe, alisema chama hicho kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kueneza uelewa wa tatizo la rushwa hususan kwa wabunge.
Hata
hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo katika kutatua tatizo la
rushwa, ni kutokana na mara zote rushwa kufanyika kwa siri na hufanywa
na watu wenye nafasi kubwa katika jamii wakiwemo wanasiasa na wachumi
hivyo kuwa vigumu kuwakamata.
Aliwataka
wabunge hao kutotumia nafasi zao ndani ya Bunge na kukemea rushwa kwa
mdomo pekee bali waoneshe dhahiri kuichukia na kupambana nayo kwa
vitendo.
Mbunge
wa Nkasi, Ally Keissy, wakati akichangia mada hiyo ya rushwa, alisema
tatizo la rushwa litamalizika endapo Mahakama na vyombo vya dola
vitachunguzwa kutokana na ukweli kuwa kesi nyingi za rushwa
zimefunguliwa, lakini hazishindi.
0 comments:
Post a Comment