SERIKALI
imeipatia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Shilingi Billioni
2.3 (Bilioni mbili na milioni mia tatu) kwa ajili ya kuwalipa waliokuwa
watumishi wa muda wa mamlaka hiyo, wapatao 597, waliosimamishwa kazi
hivi karibuni.
Malipo
hayo yanahusisha mishahara yao ya miezi minne, ukiwemo mshahara wa
mwezi mmoja wa notisi ya kusimamishwa kazi, pamoja na malimbikizo ya
madeni yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kabla
ya NIDA kuwalipa watumishi hao fedha hizo, Wizara ya Fedha na Mipango
iliamua kufanya uhakiki ili kujiridhisha kama madai hayo yalikuwa
sahihi.
Uhakiki
huo ulihusisha mahojiano ya ana kwa ana na watumishi hao pamoja na
kupitia nyaraka mbalimbali zikiwemo majalada, mikataba ya ajira,
madaftari ya mahudhurio, taarifa za kazi za kila siku na namba zao za
akaunti za benki zilizokuwa zikitumika kulipa mishahara.
Katika
uhakiki huo imebainika kuwa kulikuwa na kasoro ama changamoto kadhaa
zikiwemo za kimikataba kati ya NIDA na watumishi hao.
Wakati
wa zoezi hilo, jumla ya watumishi 597 walipaswa kuhakikiwa lakini
majina ya watumishi yaliyowasilishwa kuhakikiwa ana kwa ana kutoka NIDA,
Tanzania bara yalikuwa 565.
Hata hivyo, watumishi 516 pekee ndio waliojitokeza katika zoezi hilo na wengine 49 hawakujitokeza.
Watumishi
wa muda 32 kutoka NIDA Tanzania Zanzibar, wanaofanya jumla ya watumishi
wa Mamlaka hiyo waliosimamishwa kazi kufikia 597, walihakikiwa kwa
kupitia majalada yao yaliyoko ofisi za NIDA Makao Makuu, na kubaini
mikataba yao haikuwa na kasoro.
Kwa
mantiki hiyo watumishi 427 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar
ndio waliokidhi vigezo vya kulipwa stahili zao za kuachishwa kazi.
Aidha,
watumishi wengine 121, walibainika kuwa na kasoro mbalimbali ambazo
zinapaswa kurekebishwa na Menejimenti ya NIDA kabla ya kufanya malipo
hayo.
Baadhi
ya kasoro zilizobainika katika uhakiki huo ni pamoja na kukosekana kwa
mikataba na majalada yao katika Ofisi ya mwajiri, kukosekana majina yao
kwenye daftari la mahudhurio kazini, kuwa na utata kwenye mikataba
(kutofautiana tarehe na sahihi za wahusika), kufanana kwa namba za
majarada, na kukosekana kwa barua za kusitishwa kazi.
Wizara
ya Fedha na Mipango imemaliza kazi yake ya uhakiki na kwamba jukumu la
kuwalipa watumishi wa NIDA wanaostahili limeachwa mikononi mwa
menejimenti ya NIDA.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
13 Mei, 2016
0 comments:
Post a Comment