Sunday, May 1, 2016

Serikali Yaiagiza Mamlaka ya Bandari na TRA Kubaini Chanzo cha Kupungua kwa Shehena ya Kontena Zinazoingia Nchini

SERIKALI imeziagiza Mamlaka ya Bandari-TPA, na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kufanya uchambuzi wa kina ili kubaini sababu za kupungua kwa shehena ya kontena zinazoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dokta Philip Mpango, ameliambia Bunge mjini Dodoma, jana tarehe 30, Machi, 2016 kwamba taarifa zilizopo zinaonesha kwamba uingiaji wa mizigo inayopelekwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Malawi na Zambia kupitia bandari hiyo, umeshuka.

Alisema katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu kontena zilizopelekwa nchini Congo zilishuka kutoka 5,529 hadi 4,092, wakati yale yaliyokuwa yakipelekwa nchini Malawi yalishuka kutoka kontena 337 hadi 265, huku yale ya Zambia yakishuka kutoka 6,859 hadi kufikia 4,448.

Hata hivyo, Dokta Mpango aliwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba kushuka kwa kiwango cha kontena ziendazo nchi jirani kupitia  Bandari ya Dar es salaam, hakujaathiri malengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.Alisema sababu mojawapo ya kushuka kwa idadi ya kontena zinazopitia bandari ya Dar es slaam zinachangiwa na kuporomoka kwa uchumi wa China ambao umeathiri nchi mbalimbali duniani ikiwemo  Tanzania.

"lakini naziagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania-TPA na Mamlaka ya Mapato-TRA, zichambue mwenendo huo ikilinganishwa  na nchi nyingine" alisisitiza Dokta Mpango.Alilieleza Bunge pia kwamba, Tanzania haitozi kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kontena zinazosafirishwa kutoka bandari hiyo kwenda nchi jirani hivyo hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuzikwaza nchi jirani kutumia bandari ya Dar es salaam
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger