Monday, May 2, 2016

Mtoto Wa Miaka Mitatu Afariki Dunia Papo Hapo Baada Ya Kugongwa Na Gari

Mtoto wa miaka mitatu aliyefahamika kwa jina la JANET PONSIAN mkazi wa Matemela Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na Gari yenye namba za usajili T.957 CWJ aina ya Isuzu Journey ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la ELIABU MYEKO (33) mkazi wa Makambako Mkoa wa Njombe.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 01.05.2016 majira ya saa 17:45 jioni huko katika Kijiji cha Matemela, Kata ya Ipwani, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.

Aidha chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa Dereva wa Gari hilo. Dereva alikimbia mara baada ya tukio na jitihada za kumtafuta kwa kushirikiana na mmiliki wa Gari zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Kituo cha Afya Ipwani Wilayani Mbarali kwa uchunguzi wa kitabibu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi EMANUEL G. LUKULA anatoa wito kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Aidha anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa dereva huyu azitoe kwa mamlaka husika ili akamatwe.

Katika Misako:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja mkazi wa Matemela aliyefahamika kwa jina la HUSSEIN BAKARI (59) baada ya kukutwa na miche 25 ya Bhangi akiwa amepanda kwenye bustani yake ya mbogamboga.

Mtuhumiwa alikamatwa katika msako uliofanyika mnamo tarehe 01.02.2016 majira ya saa 16:00 jioni katika Kijiji cha Mayota, Kata ya Lugelele, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.

Aidha katika msako mwingine, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la WILSON PHILIP (19) mwendesha Pikipiki @ bodaboda, mkazi wa Msasani anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya akiwa na Bhangi yenye uzito wa Gram 10.

Mtuhumiwa alikamatwa na askari katika msako uliofanyika mnamo tarehe 01.05.2016 majira ya saa 17:05 jioni huko Mtaa wa msasani, Kata ya Bagamoyo, Tarafa ya Tukuyu Mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamiliki.

Imesainiwa na:
(EMANUEL G. LUKULA – ACP)
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger