ZIKIWA ni siku chache
zimepita tangu staa wa Muziki wa Bongo Fleva, Snura Mushi kufungiwa
video yake ya Chura na kutakiwa kuitengeneza upya, Video Queen, Gift
Stanford ‘Gigy Money’ naye amejikuta akikumbana na rungu la
Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) kufuatia kusambaza kava la video ya
wimbo wake mpya lenye picha yake inayomuonesha akiwa mtupu.
Kava hilo la wimbo wake wa Supu ambao
alitarajia kuuachia jana, alilisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya
kijamii ambapo mashabiki walioiona kwa mara ya kwanza walishangazwa na
kitendo hicho kwani picha yake haikumstiri mwili kama yalivyo maadili ya
Kitanzania.
“Yaani hawa wasanii ni sikio la kufa,
Gigy ameweka kava hili ambalo lina picha yake ya nusu utupu kabisa na
limesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, hajajifunza kwa
mwenzake Snura?” alihoji mdau mtandaoni.
Walipotafutwa Basata na kuulizwa juu ya
video queen huyo, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema
wao wanasimamia maadili ya Kitanzania hivyo kama Gigy amekiuka, wanampa
onyo asiuachie wimbo huo hadi atakapoufanyia marekebisho.
“Kwanza huyo Gigy Money hatumtambui
kabisa hapa baraza maana hajajisajili kama msanii na sheria ya mwaka
1984 inasema mtu yeyote hatakiwi kufanya kazi ya sanaa bila kujisajili
hivyo hata hao ma-video queen wanatakiwa wajisajili maana hatuwatambui.
“Mtu akikiuka maadili, hatumvumilii na
asitegemee kazi yake kupigwa katika vyombo vya habari wala mitandao,
tunawasihi wasanii kutoa kazi zenye maadili ili kuepuka usumbufu,”
alisema Mngereza.
Alipotafutwa Gigy kuhusiana na suala hilo, alisema:
“Mimi najua ma-video queen hatuhusiani
na mambo ya Basata na niseme tu wimbo wangu wuko ndani umetulia, kava
lisiwatishe ila nitaenda Basata kufuata utaratibu,” alisema Gigy.
0 comments:
Post a Comment