Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Vincent Mashinji
ameponda mtindo wa utawala wa Rais John Magufuli wa utumbuaji wa majipu
akisema umekosa dira na kinachoendelea ni utashi wa kisiasa na
kukurupuka.
Kazi
kubwa aliyoifanya Rais Magufuli tangu aingie madarakani, katika kipindi
cha miezi sita sasa ni kubana matumizi ya fedha za umma kwa kufuta
safari za nje za watumishi, kuzuia mikutano kufanyika mahotelini,
kuhimiza mamlaka husika kukusanya kodi, kupambana na watumishi hewa,
kuwasimamisha au kutengua uteuzi wa watendaji aliodai kuwa ni wazembe na
walioshindwa kwenda na kasi yake pamoja na kuwashughulikia wala rushwa
na wahujumu uchumi.
Katika namna inayoonekana ni kufuata upepo wa kisiasa, Rais Magufuli huwatumbua baadhi ya watendaji kwenye mikutano ya hadhara.
“Kuna
vitu vingi vinafanyika lakini hatujui kipi ni kipi na wapi tunaelekea.
Kuna mambo mengi yanafanyika, lakini hakuna hata mtu mmoja katika nchi
hii anayejua Taifa hili lina mpango gani na linaelekea wapi,” Mashiji anakaririwa na gazeti la Mwananchi.
Huku
akifananisha utawala wa Rais Magufuli na wa mtangulizi wake Jakaya
Kikwete, Dk Mashinji alisema walau ahadi ya “Maisha bora kwa kila
Mtanzania” ilikuwa inaeleweka hata kama haikutekelezeka.
“Rais
Kikwete alitwambia Maisha bora kwa kila Mtanzania na tulijua maisha
hayo yanapatikana kwa kupambana wenyewe na tulipambana. Lakini sasa
hatujui tunaelekea wapi. Hapa kazi tu! Umemfukuza huyu kazi halafu nini
kitaendelea? Keshaondoka kakuacha, unaajiri mwingine? Tunahitaji mtu wa
kujibu hayo maswali. Nchi yote sasa inavurugwa. Halmashauri
zinavurugwa,” alisema.
Katibu
mkuu huyo alisema kwa sasa kila kitu kinavurugwa jambo ambalo ni hatari
kwa mustakabali wa nchi na kwamba inaonekana wazi nchi inaelekea sehemu
ambayo mbele kuna giza.
Akitoa
mfano wa mfumo ulivyobadilika alisema hivi sasa wakurugenzi wa
halmashauri wametangaziwa kusitisha mawakala wote wanaokusanya ushuru
badala yake wakusanye wenyewe.
“Hivi tujiulize halmashauri ina wafanyakazi wangapi ambao wana uwezo wa kukusanya mapato yake? Huku ni kudanganyana,” alisisitiza Dk Mashinji.
Hata hivyo, Dk Mashinji alisema hawapingi anachokifanya bali tofauti yao na Rais Magufuli ni namna ya kukabiliana na jambo.
“Sisi
tunaamini katika mfumo na siyo mtu. Huwezi leo kuniambia meya anaiba
Sh5 bilioni halafu chama kisijue. Kwa nini chama kisimwondolee udhamini
kabla?” alihoji.
“Anachofanya
sasa ni kudhibiti na siyo kurekebisha mfumo. Rais Magufuli hana dhamana
na Mungu, asipokuwepo sioni wa kuendeleza falsafa zake. Kwa nini kusiwe
na mfumo madhubuti ambao upo kisheria na kila mmoja aujue na kuufuata?”
alieleza.
0 comments:
Post a Comment