MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, amesema wametenga kiasi
cha shilingi bilioni 4.5 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya
kuwasaidia kiuchumi wanawake na vijana wa Manispaa hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi sehemu ya fedha
hizo, Jacob alisema hadi kuwafikia walengwa zitatolewa kupitia Benki ya
Wananchi Mkoa wa Dar es Salaam (DCB).
Alisema fedha hizo ni asilimia 10 ya mapato yote ya ndani ya Manispaa
hiyo ambayo inatakiwa kutoa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana
katika shughuli zao za kiuchumi.
Alisema jana amekabidhi Sh 19,500,000 kwa vikundi sita na kwamba zoezi
hilo la ugawaji wa fedha za mkopo kwa ajili ya kujikwamua kimaisha
litakuwa endelevu ili kutekeleza agizo la Serikali.
“Ndugu wananchi fedha zipo kwa ajili yenu naomba mchangamkie fursa kwani
ni mkopo ambao hauna masharti magumu na riba yake ni asilimia 10 tu
ambayo ni rahisi kuliko benki zote,” alisema Jacob.
Alisema fedha hizo ni za awamu ya kwanza na kwamba katika awamu ya pili
wanatarajia kutoa Sh bilioni 5.5 ambazo zitatokana na bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2016/2017.
Jacob alizitaja baadhi ya kata alizozikabidhi hundi kwa ajili ya mikopo
na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni Kata ya Kigogo (7,700,000),
Kata ya Kilungule B (3,000,000), Kata ya Saranga Mtaa wa Kimara B
(4,100,000), Kata ya Saranga Mtaa wa Stop Over (2,100,000), Kata ya Goba
Mtaa wa Goba (2,650,000) na Kata ya Goba Mtaa wa Mwembe Dole.
Naye Meneja Mikopo wa benki ya DCB, Maria Kabeho, alisema wahitaji wote
wanatakiwa kujiunga katika kikundi cha watu watano ili waweze kupatiwa
mkopo.
“Tunachotaka sisi ni uaminifu na uthubutu wa vikundi ili tuweze
kuwapatia mikopo,” alisema Maria.
Kwa upande wake, Emmanuel Abdul ambaye ni kiongozi wa madereva wa
bodaboda katika Kata ya Goba Mtaa wa Goba, alisema mkopo huo utawasaidia
kutanua mitaji yao na kwamba wanaomba mikopo hiyo iwe endelevu.
Pia alisema wanaomba wasaidiwe wawe wanafika mjini kupeleka abiria.
0 comments:
Post a Comment