Monday, April 25, 2016

CAG kuanika ufisadi leo, ni ule wa NSSF, deni la taifa pamoja na watumishi hewa

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Assad 

 Machi 28, mwaka huu, Rais Magufuli alipokea ripoti ya CAG, Prof. Mussa Assad, Ikulu jijini Dar es Salaam
Katika mahojiano na Nipashe mjini hapa jana mchana, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya, alisema ripoti ya CAG itawasilishwa bungeni leo asubuhi.

“Ratiba inaonyesha Ripoti ya CAG itawasilishwa kesho (leo) saa 3:00 asubuhi wakati Bunge litakapokuwa linapokea hati za kuwasilishwa mezani,” alisema Owen jana
Miongoni mwa hoja zinazotarajiwa kuwa gumzo katika ripoti hiyo ni madai ya uwapo wa ufisadi katika Mfuko wa Kijamii wa NSSF, ‘mchwa’ wa fedha za maendeleo katika halmashauri hasa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, kukua kwa kasi kwa deni la taifa na watumishi hewa serikalini.

UFISADI NSSF

Hivi karibuni kuliibuka madai ya kuwapo kwa ufisadi wa fedha za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF unaodaiwa kufanywa na waliokuwa viongozi wa mfuko huo. Ripoti ya CAG inatarajiwa kuanika ukweli kuhusu tuhuma hizo.

DENI LA TAIFA

Jumanne ya wiki iliyopita, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilimtaka CAG kufanya ukaguzi maalum (Special Audit) wa deni la taifa na kupeleka taarifa ya ukaguzi huo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa baada ya kubaini deni hilo limekua maradufu kutoka 2010 hadi 2015

Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani – Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde, alisema hali ya deni la taifa inatisha na Bunge linapaswa kushtuka.

Silinde alisema nchi itafilisika kama Ugiriki, ikiwa Bunge halitachukua hatua madhubuti za kuisimamia serikali.
Alisema deni la taifa limekuwa na kufikia Dola za Marekani bilioni 19.141 (Sh. trilioni 41.536). Alisema deni liliongezeka maradufu 2015 baada ya serikali kukopa Dola bilioni 3.846 (Sh. trilioni 8.347

“Mwishoni mwa Juni, 2010, jumla ya deni la Tanzania lilifikia dola bilioni 9.9 (Sh. trilioni 13.6) kulingana na thamani ya dola kipindi hicho). Miaka mitano baadaye, deni limefikia Sh. trilioni 41.5, lazima Bunge tushtuke,” alisema Silinde.

“Fedha zilizokopwa kuanzia 2010 hadi 2015 zilifanyia miradi ipi ya maendeleo? Mikopo hii ina riba kiasi gani, tumeweka nini kama dhamana ya kupatiwa mikopo au ile minong’ono mitaani ya vitalu vya gesi?, Alihoji na kuongeza:”Mkopo mkubwa wa mwaka 2010 ambao ni sawa na asilimia 5.9 ya deni lote ulitumika kufanyia jambo gani? Fedha hizi zimetumika kugharamia miradi gani au ndiyo EPA ya Uchaguzi Mkuu wa 2015?,” Alihoji Silinde

MCHWA FEDHA ZA MAENDELEO

Tuhuma za kukosekana kwa uadilifu katika matumizi ya fedha za maendeleo zimezikumba halmashauri nyingi, huku baadhi ya watendaji wake ‘wakitumbuliwa.’
Mchwa wa fedha za maendeleo wamekuwa wakibaini katika ripoti zilizopita za CAG kuhusu halmashauri mbalimbali nchini, hivyo macho na masikio ya wengi yanatarajiwa kuelekezwa kwenye changamoto hiyo.

WATUMISHI HEWA

Wakati wa kuwaapisha wakuu wa mikoa, Rais Magufuli aliwaagiza kuhakikisha wanawasaka watumishi hewa wanaolipwa mamilioni ya shilingi, changamoto ambayo ilimng’oa madarakani aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela.

Ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15, ilibainisha kuwapo kwa kadhia hiyo na leo inatarajiwa kuanika kiasi cha fedha ambacho Tanzania imepoteza kutokana na watumishi hewa.

Source: Nipashe
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger