WAKATI Kambi ya Upinzani Bungeni ikiendelea na msimamo wake wa
kutochangia mijadala ya Bunge la Bajeti inayoendelea bungeni mjini
dodoma, bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/17 itapitishwa leo
jioni.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema
Ijumaa kuwa wabunge wa upinzani watakuwa wanaingia kwenye Ukumbi wa
Bunge, lakini hawatachangia vikao vya bajeti mpaka pale hoja zao
zitakapojibiwa.
Mwenyekiti huyo wa Chadema na Mbunge wa Hai (Chadema), alizitaja hoja
hizo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kufanya kazi bila kuwa na mwongozo
wa utendaji kazi kwa wizara mbalimbali, kuvunjwa kwa Katiba na sheria za
nchi pamoja na kupokwa uhuru na madaraka ya mhimili wa Bunge kutokana
kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja (live) ya vikao vya Bunge.
Licha ya upinzani kususa, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema
vikao vya Bunge vitaendelea kama vilivyopangwa na kwamba leo watamalizia
mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu makadirio ya
mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/17
iliyowasilishwa bungeni Ijumaa.
Chenge alisema hotuba hiyo itajadiliwa kwa siku mbili (Ijumaa na leo),
kabla ya wabunge kuamua kuipitisha ama kutoipitisha leo jioni.
Chenge ambaye aliongoza kikao cha Bunge Ijumaa jioni, pia aliishauri
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iende mahakamani kupatiwa msaada wa
kisheria akieleza kuwa hoja zao zilikuwa na tuhuma nzito kwa serikali.
MAMBO MUHIMU:
Tume Dawa za Kulevya
Katika mwaka wa fedha 2016/17, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, alisema
serikali itakamilisha utaratibu wa kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulenya ili kuongeza ufanisi.
Alisema mamlaka hiyo itashirikiana na Jeshi la Polisi kubaini mtandao wa
wahalifu ndani na nje ya nchi wanaojihusisha na uingizaji wa dawa za
kulevya na kuwafikisha wahusika mahakamani.
TUME YA UCHAGUZI
Majaliwa pia aliiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya tathmini ya
kina kubaini sababu zilizofanya wapiga kura zaidi ya milioni saba
waliojiandikisha kupiga kura, kutoitumia haki yao kikatiba.
Alisema itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwa kuwa wananchi wana wajibu
wa kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka.
Aliongeza kuwa tathmini itasaidia kubaini iwapo kuna vikwazo
vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili viondolewe kukuza
demokrasia nchini.
"Idadi ya wapiga kura walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015 ilikuwa 23,161,440 sawa na asilimia 96.9 ya
makadirio. Waliopiga kura ni 15,596,110 sawa na asilimia 67.3 ya
waliojiandikisha.
Naiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya tathmini ya kina kubaini
sababu zilizofanya zaidi ya watu milioni saba kutotumia haki yao ya
kikatiba," alisema Majaliwa.
DENI MIFUKO YA JAMII
Majaliwa pia, alisema serikali inaendelea kulipa deni la Sh. bilioni
840.4 linalotokana na miradi ya serikali iliyogharamiwa na Mifuko ya
GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF, huku akieleza kuwa kwa sasa ni asilimia
6.5 tu ya Watanzania wanaofikiwa na huduma za Hifadhi za Jamii.
ATOA AGIZO HALMASHAURI
Waziri Mkuu pia aliwaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waliokamata
mbao ndani ya halmashauri zao kuzitumia kutengeneza madawati na siyo
kuzipiga mnada.
Alisema Suma JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza madawati
80,000 yatakayotolewa kwa majimbo yote (kila jimbo madawati 300)
kutokana na Sh. bilioni sita zilizookolewa na uongozi wa Bunge kwa
kubana matumizi.
RUSHWA KUBWA 10
Kadhalika, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444
zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10
za rushwa kubwa.
0 comments:
Post a Comment