Ili kuondoa shaka miongoni mwa wananchi kutokana na tetesi zinazosambazwa juu ya ubora wa kalamu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kila mtu anaruhusiwa kuja na kalamu yake kupigia kura Oktoba 25, mwaka huu.
Kauli
hiyo imetolewa jana na NEC wakati ilipofanya mkutano wake na wahariri wa
vyombo vya habari nchini ikiwa ni siku ya tatu ya kukamilisha utaratibu
wa kuzungumza na wadau wa uchaguzi baada ya kufanya hivyo kwa
wawakilishi wa walemavu na wamiliki wa vyombo vya habari nchini.
Akisisitiza
juu ya ushiriki wa wadau kutoa elimu ya mpiga kura, Mwenyekiti wa NEC,
Jaji Lubuva amesema kipindi hiki cha kampeni kimeshuhudia kuzuka kwa
maneno mengi yasiyokuwa na uhakika ambayo yanawachanganya wananchi.
“Kalamu
yoyote inaruhusiwa kupigia kura hivyo watu wasiogope kwenda na kalamu
zao ila wasiokuwa nazo watatumia zetu tulizoziandaa. Hazifutiki kama
inavyosemwa huko mitaani,” amesema Jaji Lubuva.
Ametumia
nafasi hiyo pia kubainisha mkakati wa kuzuia uwezekano wowote wa wizi
wa kura kama inavyosemwa na baadhi ya wagombea na viongozi wa vyama vya
siasa na kutoa wito kwa mtu au taasisi yoyote inayoona mwanya wa hilo
kujitokeza ili hatua stahiki zichukuliwe.
Vile
vile amewataka wanasiasa wote kuachana na maneno machafu wawapo
majukwaani pamoja na kushambulia tume hiyo au baina ya wenyewe kwa
wenyewe na badala yake wajikite kwenye kunadi sera zao.
“Tunaumizwa
sana na matumizi ya maneno kama ‘tume inaandaa bao la mkono’ kwenye
vyombo vyenu. Hakutakuwa na wizi na sisi tunaamini ushindi utatokana na
wingi wa kura alizopata mgombea husika,” amesema na kuongeza:
“Kama
chama cha siasa kimeishiwa sera za kunadi kwa wananchi basi ni vyema
kikampumzisha mgombea wake na kusubiri siku ya uchaguzi badala ya kutoa
lugha zisizofaa. Matumizi ya kauli za matusi, dhihaka au kejeli dhihi ya
wagombea wengine ni kinyume na maadili ya uchaguzi. Hata kuituhumu tume
bila kutoa ushahidi siyo jambo jema na kutowatendea haki wananchi.”
Mwenyekiti
huyo ametoa kauli hizo baada ya kupata michango kutoka kwa wahariri
waliomueleza changamoto walizonazo katika kuruhusu matumizi ya baadhi ya
maneno yanayotolewa majukwaani.
0 comments:
Post a Comment