Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa ameeleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kuwapiga mabomu wananchi wa Tanga waliokuwa wakitoka kwenye mkutano wake.
Lowassa
alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Korogwe baada
ya juzi kulazimika kuvunja mkutano wake kutokana na wingi wa watu na
kusababisha wananchi wengi kuzimia mjini Tanga.
Baada
ya kuvunja mkutano huo, polisi walipiga watu mabomu ili kuwatawanya
jambo ambalo Lowassa alisema limemsikitisha na kuwaomba waache kufanya
hivyo na badala yake watoe ushirikiano kwa wananchi.
“Nasikitika polisi kupiga mabomu. Tushirikiane katika jambo hili ili kuondoa vurugu,” alisema Lowassa huku akiwashukuru wananchi wa Tanga kwa mapokezi makubwa aliyoyapata.
Lowassa,
ambaye jana alifanya mikutano ya aina yake akielekea Dar es Salaam kwa
gari, alisimamishwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wametanda
barabarani katika Jimbo la Muheza na kuhutubia akiwa juu ya gari akisema
anahitaji kura za kutosha ili aweze kuleta mabadiliko ambayo wananchi
wanayahitaji.
Wananchi
hao wa Muheza walimtaka Lowassa awaeleze atafika lini kufanya mkutano
mkubwa hapo na atawasaidiaje kutatua tatizo la kutozwa ushuru kwa vitu
vidogovidogo.
Lowassa
aliahidi kulishughulikia tatizo hilo la ushuru kwa kuliwekea utaratibu
maalumu atakapoingia Ikulu na kwamba kabla ya kampeni kuisha, atafika
Muheza kuzungumza na wananchi hao.
Akiwa
njiani kwenda Korogwe, Lowassa alikutana na umati mkubwa wa watu
barabarani ambao walikuwa wakielekea Korogwe mjini ambako alihutubia na
kuwaeleza kwa nini ameamua kugombea urais.
Aliwaambia
wakazi hao kuwa umaskini umekithiri na mambo kuwa hovyo, hivyo ameamua
kugombea ili kuyashughulikia na atawasaidia katika elimu, afya na
kilimo.
“Hapa mkoani kwenu nitafufua Bandari ya Tanga ambayo ndiyo itainua uchumi wa mkoa huu,” alisema Lowassa.
Akitokea
Korogwe kuelekea Dar es Salaam, umati mkubwa wa wananchi ulisimamisha
msafara wake katika eneo la Michungwani jambo lilimfanya asimame tena na
kuhutubia kwa dakika saba akiwaomba wamchague ili aboreshe sekta ya
elimu na kuifufua Bandari ya Tanga.
Msafara
mgombea huyo ulipofika Kabuku ulisimamishwa tena na polisi walifanya
kazi kubwa kuwaweka wananchi pembeni huku magari yakikaa kwenye foleni
na kusubiri Lowassa ahutubie.
Wananchi hao walisema kuwa kuanzia asubuhi walikuwa wanasubiri ‘mabadiliko’.
Lowassa aliwaomba kura wananchi hao kwa kuwahoji, “mtanipa kura zenu?” nao wakajibu; “tutakupaaaaaaa”.
Lowassa alisema atawatatulia tatizo la maji ambalo linawakumba wakazi wa Kabuku kwa muda mrefu.
Wananchi
hao walimwonyesha maji wanayokunywa jinsi yalivyo machafu na baada ya
kuyaona alisema wakimpa kura, atahakikisha wanapata majisafi na salama.
Akiendelea
na safari, alikuta umati mwingine wa wananchi alipofika Komkonga ambako
aliwaahidi kushughulikia tatizo la maji na hospitali, mambo ambayo
wananchi wa hapo walimweleza kuwa ni kubwa kwao.
Alitumia dakika tatu kuwaomba kura ili akiwa rais, awatatulie matatizo yao. Baadaye alisimama na kuhutubia eneo la Mkata.
0 comments:
Post a Comment