MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi),
ametoa siri ya moyoni kwamba kashfa ya sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta
Escrow lilimkutanisha na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilali ili
kumueleza ukweli wa sakata hilo.
Vilevile, amesema Dk. Bilal ndiye
kiongozi pekee wa Serikali ambaye alionesha dhahiri kuwa aliguswa kutokana na
wizi huo wa fedha za umma.Kafulila alisema hayo wakati
akipokea tuzo ya Mtanzania mwenye maono mapevu iliyotolewa juzi na Taasisi ya
Dream Success Enterprises, jijini Dar es Salaam.
Alisema ametoa siri hiyo sasa
kutokana na ukweli kuwa kiongozi huyo wa pili kwa madaraka nchini kumuita na
kufanya mahojiano naye kwa saa nne kuanzia saa nne usiku hadi saa nane ili
kumueleza kuhusu sakata hilo hiyo ikiwa ni baada ya kupotoshwa na watendaji wa
Serikali.
Mbunge huyo alisema, baada ya
kuitwa alipata wasiwasi mkubwa kwani haijawahi kutokea, akalazimika kuwataarifu
ndugu zake kuwa ameitwa na makamu wa rais hivyo asiporejea wajue kwamba aliitwa
na kiongozi huyo.
Kafulila alisema baada ya kufika
makamu wa rais alitaka kujua nini kipo katika sakata hilo hiyo ikiwa ni baada
ya viongozi wanapokutana na mataifa yaliyoendelea, wahisani na mashirika ya
fedha wanashindwa kuelewana hali ambayo ilichangiwa na upotoshaji wa watendaji.
Alisema alipofika alimueleza kila
kitu kuhusu sakata hilo la Escrow ndipo Dk Bilal akapata ufahamu na kukiri kuwa
alikuwa anadanganywa na watendaji wake hivyo kupatwa na huzuni kubwa kwa
kuongea uongo mbele ya wahisani ambao walikuwa wanajua kila kitu.
“Katika sakata la Escrow kuna
jambo ambalo sijawahi kulisema leo (juzi) nasema kwa sababu naona watu
waadilifu hawathaminiwi, nakumbuka siku moja saa nne usiku niliitwa na Makamu
wa Rais Dk. Bilal hadi sa nane ambapo alitaka nimueleze kila kitu ninachokijua
kuhusu Escrow ili aweze kujieleza mbele ya watu mbalimbali jambo ambalo hakuna
kiongozi mwingine wa Serikali alifanya hivyo.
“Nilikuwa na taarifa yenye
takribani kurasa 600 nilitumia saa nne kumueleza kila jambo, ambapo kimsingi
alionekana kuumia sana na aliniuliza hivi kweli rais anajua haya au na yeye
yupo kama mimi huku akitikisa kichwa,” alisema Kafulila.
Mbunge huyo alisema
kilichoonekana ni wazi kuwa watendaji wa Serikali waliamua kumdanganya au nao
walikuwa hawajua jambo ambalo lilimsukuma kutaka kujua ukweli ulivyo.
Alisema pamoja na maelezo yote
ambayo aliyatoa kwa Makamu wa Rais saa tisa usiku alifuatwa na watu ambao
walikuwa na magari matatu wakimtaka asiseme yote ambayo yapo katika taarifa
yake kwani mengine ni makubwa na hatari.
Mbunge huyo alisema siku hiyo
umeme ulikatika, lakini watu hao walimpigia simu muda wote na kumtaka waonane
aligoma ila baadae alikubali pamoja na ukweli kuwa umeme haukuwepo.
Kafulila alisema kutokana na
uzalendo huo ambao Dk. Bilal alionesha aliamini kuwa ni mmoja wa Watanzania
wazalendo na waadilifu, lakini katika jambo la kushangaza katika mchakato wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitisha majina ya wagombea walimkata bila kuingia
hata tano bora.
“Kutokana na uadilifu wa yule
mzee nilibakiwa na mshangao pale, ambapo CCM kupitia kamati yake ya maadili
kumkata sijui wanatumia kigezo gani kuangalia uadilifu,” alisema.
Sakata la Escrow liliibuliwa na
Kafulila ndani ya bunge, ambapo baadae lilifikishwa katika Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilifanyia uchuguzi na kutoa taarifa
iliyosababisha bunge kutoka na maazimio nane ili Serikali itekeleze.
Baadhi ya maazimio hayo ni
Serikali kuwawajibisha Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme
Tanzania(Tanesco) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika
miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya
Pan African Power Solutions Ltd. (PAP), na VIP Engineering & Marketing
(VIP).
Pia, azimio lingine lilikuwa ni
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo
vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria,
kwa mujibu wa sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati
kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya
Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya
jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;
Bunge pia liliazimia Waziri wa
Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredirick Werema, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;
Aidha azimio lingine la bunge
lilikuwa ni Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa
vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao
Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge ambao walikuwa ni Andrew
Chenge, William Ngeleja na Victor Mwambalaswa.
Azimio lingine lilikuwa ni
kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya
Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi
na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pia, azimio lingine lilikuwa ni
mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania)
Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka
za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika
Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu
(institutions of money laundering concern).
Bunge liliazimia pia, Serikali
iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda Takukuru kwa
lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti
vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa
taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aidha Bunge linaazimia kwamba
Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
Azimio la nane la Bunge ni
Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote
vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa
ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme jambo ambalo halikufanyika na
kusababisha Kafulila kuomba muongozo ndani ya bunge kila mara kuhusu lini
taarifa hiyo itawasilishwa.
Source: Jamboleo
0 comments:
Post a Comment