Tanzania imeadhimisha siku ya hedhi duniani, ambapo wizara ya elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamekubaliana kuandaa na kusimamia sera inayoondoa vikwazo kwa watoto wa kike katika masomo yao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Madina Kemilembe, alisema kukosekana kwa miundombinu rafiki mashuleni kunasababisha wanafunzi kutohudhuria masomo.
Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na salama pamoja na vyumba mahsusi vya kubadilishia nguo , hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika hedhi mashuleni kunachangia utoro.
“Nawashukuru wadau Water Aid, Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), Kasole Secrets pamoja na wengine kwa kuisaidia serikali kuandaa mazingira rafiki kwa watoto wetu kwa kuwajengea vyumba vya kubadilishia na kuhakikisha upatikanaji wa pedi kwa baadhi ya shule,” alisema Kemilembe.
Alisisitiza juu ya utoaji wa elimu kwa wazazi na wanafunzi wa jinsia zote ili kuondoa unyanyapaa ili kuboresha mazingira ya kusoma kwa mtoto wa kike. Naye Mkurugenzi wa Water Aid, Ibrahim Kabole, alisema kuna uelewa mdogo pamoja na mila potofu zinazofanya jambo la hedhi kuonekana ni la aibu.
Afisa Elimu Mkuu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi Madina Juma, akihutubia wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani yaliyofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania jana jijini Dar es Salaam katika viwanja vya mnazi mmoja. Kauli Mbiu ya mwaka huu inaeleza "Usisite kuzungumzia hedhi".
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye maandamano ya kuadhimisha siku ya hedhi duniani yaliyofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania jana jijini Dar es Salaam.Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaeleza "Usisite kuzungumzia hedhi".
0 comments:
Post a Comment