Friday, November 1, 2013

"SIOGOPI HOJA YA KUNG'OLEWA USPIKA..WACHA WAKUSANYE HIZI SAINI".....ANNE MAKINDA

Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.

 
Kadhalika Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.

Kanuni si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jana.

Wakati Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.

Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.

Hoja nyingine ni kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya bajeti wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.

Jana Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.

Makinda akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la sasa.

Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii haikuwapo na wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,” alisema Makinda na kuongeza:

Kamati hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda mfupi wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee Chenge ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.

Kuhusu posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena kwa kibali chake.

Lazima walete maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,” alisema.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger