Friday, October 18, 2013

NDEGE YA FASTJET YASHINDWA KUTUA MWANZA BAADA YA UMEME KUZIMIKA....


KUZIMIKA kwa taa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza juzi kulisababisha ndege ya fastjet kushindwa kutua na kulazimika kurejea jijini Dar es Salaam.

Inaelezwa kwamba ndege hiyo iliyopaswa kutua saa 2 usiku kwenye uwanja huo ikitokea jijini Dar es Salaam, ilishindwa

 kutua na kulazimika kuzunguka hewani mara tano, hali inayodaiwa kuleta taharuki miongoni mwa abiria.

Habari zinadai kuwa kukosekana kwa umeme katika uwanja huo kulisababisha kutokuwapo kwa mawasiliano, hivyo kuzua tafrani kubwa kwa baadhi ya abiria.

Baadhi ya abiria waliosafiri na ndege hiyo waliieleza Tanzania Daima kwamba wengi walikumbwa na hofu ya kuzama katika Ziwa Victoria.

“Tuliogopa sana baada ya kuona ndege imeanza kuzunguka zunguka angani, na tukahofia kuwa huenda tukatumbukia ziwani, maana uwanjani hakukuwa na umeme.

“Nilianza kusali huku mapigo ya moyo yakinienda mbio sana. Maana rubani angeweza kushuka ziwani kwa kuona taa za wavuvi,” alisema abiria mmoja ambaye hakutaja jina lake.

Hata hivyo, baadhi ya abiria na wadau wengine wa usafiri, akiwamo Mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje na Meneja wa Shirika la Bima la Jubilee Mkoa wa Mwanza, Jared Owando, walieleza kusikitishwa na taarifa za kukatika kwa umeme kwenye uwanja wa ndege.

Walisema kwamba, kitendo hicho kinapaswa kudhibitiwa, ikiwa ni pamoja na uongozi wa uwanja huo kuwajibika kikamilifu, ili tatizo hilo lisijirudie tena, kwani hali hiyo ni hatari katika usalama wa abiria na ndege kwa ujumla: “Siku hiyo mimi nilifika Mwanza mapema usiku na ndege ya Precision kutoka Dar. Lakini baadaye nikaarifiwa kwamba kuna ndege imelazimika kurejea Dar es Salaam kwa sababu uwanja una giza. Sasa najiuliza, hakuna jenereta uwanjani hapo?” alisema Jared.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Easter Madale, alipoulizwa jana kwa njia ya simu kuhusiana na tatizo hilo, alikiri kutokea hitilafu ya umeme hivyo ndege hiyo kupata usumbufu ikiwa angani, na kusema hilo ni tatizo la kawaida: “Ni kweli siku hiyo kulikuwa na hitilafu ya umeme, hivyo mawasiliano yakakosekana! Umeme ulikatika na jenereta la TCAA halifiki huku kwetu…na sisi hapa jenereta yetu ni ndogo haina nguvu sana,” alisema meneja huyo.

Miaka kadhaa iliyopita iliwahi kutokea ajali mbaya, baada ya ndege ya mizigo kutoka Ulaya iliyokuja kubeba samaki kutumbukia ndani ya Ziwa Victoria, kutokana na kukosekana kwa umeme na mawasiliano uwanjani hapo.

--- via Tanzania Daima
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger