Sunday, May 12, 2013

UGAIDI WAITESA CCM...

UAMUZI wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumfutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, umekiweka katika mazingira magumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa.
Mazingira hayo magumu yanatokana na kuwepo kwa taarifa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, ambaye baadhi ya wachambuzi wanasema ndiye mwasisi wa dhana ya ugaidi wa Lwakatare, alipanga kutumia kesi hii kama turufu ya kuiumiza CHADEMA inayoonekana kuwa tishio kwa chama tawala.
Vyanzo vyetu vya taarifa vinasema CCM ilitumia rasilimali nyingi kuchonga suala hili, ikitarajia kulitumia kuidhoofisha CHADEMA inayoonekana kuimarika hatua kwa hatua na kutishia mustakabali wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
CHADEMA sasa ndicho chama kinachoinyima usingizi CCM kiasi cha makada wake kupanga mbinu mbalimbali za kukiua ikiwemo kudai ni chama cha kikabila, kidini na kigaidi; mbinu ambazo huko nyuma walizitumia dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa tishio.
Licha ya mbinu mbalimbali za kuiua CHADEMA, hali ya mambo bado inaonekana kuwa ngumu zaidi kwa CCM, kwani wananchi wanaonekana kuzipuuza, na hujuma hizi zimekuwa zikivuja kabla ya kutekelezwa.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa kukwama kwa mbinu hizo za CCM ni dalili za wananchi kuchoshwa na utawala wa chama hicho na kuimarika kwa CHADEMA, ambayo imejipambanua kuwatafutia wananchi ukombozi wa pili.
Baadhi ya wanachama wa CCM wanaojipambanua kama makada makini, wamesema mbinu za kigaidi anazotumia Mwigulu na wenzake wakidhani wanaidhuru CHADEMA, zinaweza kukimaliza chama chao kwa kuwa wananchi wa sasa wana uelewa mpana kuliko miaka kadhaa iliyopita.
Majigambo ya Mwigulu
Katika hali ya kushangilia hujuma walizokuwa wamepandikiza dhidi ya CHADEMA, huku chama hicho kikisisitiza kuwa tuhuma za ugaidi zilikuwa za kupika, Mwigulu alijigamba bungeni Aprili 12 mwaka huu, kuwa ana ushahidi mzito wa ugaidi wa Lwakatare, na kwamba alikuwa tayari kuutoa popote, duniani au mbinguni.
Mwigulu amekuwa akihusishwa na mikakati ya kuimaliza CHADEMA, na inasemekana anaungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amewahi kumsifia kwa jinsi “anavyoichachafya CHADEMA”. Wadadisi wa kisiasa wanasema sifa alizopewa na Rais Kikwete zilichangia kumpatia cheo cha unaibu Katibu Mkuu wa CCM, ambacho anakitumia zaidi kufanya propaganda dhidi ya CHADEMA kuliko kujenga chama chake.
Hata hivyo, tambo zake zimeota mbawa baada ya mahakama kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashtaka ya ugaidi Lwakatare kwa hoja kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba alikusudia kutenda jinai ya ugaidi kama ilivyodaiwa na jamhuri.
CHADEMA imekuwa ikisema kuwa tuhuma hizo za ugaidi ni za kupanga kwa malengo ya kisiasa, na kwamba Mwigulu ndiye amekuwa akishirikiana na baadhi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kutengeneza video ya uongo dhidi ya Lwakatare na chama chake.
Hoja ya vyombo vya dola kubambikizia kesi wananchi imeungwa mkono na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, ambaye mara baada ya kupewa adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja, alisema ni tabia iliyoota mizizi ya polisi kuwabambikiza kesi wananchi wasio na hatia.
Wakati hoja ya kuwabambikia kesi watu ingali ikiendelea, juzi Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewatia mbaroni askari wake watatu kwa tuhuma za kumbambikia fuvu la kichwa cha mtu mfanyabiashara mmoja wakimshinikiza awape sh milioni 25 ili wamuachie.
Wakati CCM ikionekana kuhaha kutafuta mbinu za kukabiliana na CHADEMA baada ya kushindikana kwa ugaidi, Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk. Willibrod Slaa aliweka wazi kuwa chama tawala kisitarajie mbinu ilizotumia miaka ya nyuma kuudhoofisha upinzani zitafanya kazi sasa.
Dk. Slaa katika mahojiano yake na Tanzania Daima, katikati ya wiki alisema CHADEMA haitolipa kisasi kwa makada wa CCM wanaofanya mbinu chafu za kuudhoofisha upinzani.
“CCM ilizoea kununua wananchi; zamu hii itakuwa na wakati mgumu, ilizoea kuiibia CHADEMA, sasa mambo ni magumu ijiandae kwa pigo kuu,” alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa hatua ya mahakama kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi ya Lwakatare yameinusuru zaidi CCM kuliko CHADEMA, kwani kama kesi ingeendelea chama hicho cha upinzani kilikuwa kimeandaa ushahidi mkali ambao ungeiumbua CCM, serikali na Jeshi la Polisi.
Waziri afunguka
Tanzania Daima Jumapili, lilimtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe azungumzie kufutwa kwa kesi ya ugaidi na watu kubambikiziwa kesi, ambapo alisema vyombo vya dola vinatekeleza majukumu yake kulingana na taratibu walizojiwekea.
Alisema serikali haina tatizo na hukumu ya Mahakama Kuu, kwani imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria na yeyote anayehusisha na masuala ya siasa huu ni mtazamo wake.
“Mimi ndiye msimamizi wa mahakama, kwahiyo nakubaliana na hukumu ya Lwakatare, najua mahakama imetekeleza wajibu wake na kazi zake kwa mujibu wa sheria, sina tatizo na hukumu hiyo,” alisema Chikawe.
Wanasheria wanena
Akitoa maoni ya mtazamo wa kisheria kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu, wakili na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba alisema sura ya awali kabisa kuhusu mashtaka ya serikali dhidi ya Lwakatare haikuonesha ushahidi wa kutosha au mazingira ya kutendeka kwa kosa la ugaidi.
“Sijaisoma ile hukumu ya Mahakama Kuu ili kujua kwanini jaji alifikia uamuzi huo, lakini ninachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kwamba hapakuwa na ushahidi wowote wa maana wa kuthibitisha kosa la ugaidi, hapakuwa na kosa la ugaidi pale, na nadhani mahakama imezingatia ukweli huo,” alisema Bisimba.
Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatara alisema kuwa kwa sasa wanaandaa mipango ya kumtoa mahabusu kwa dhamana mteja wao, kwani shtaka lililobaki lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Lwakatare sasa amebaki na shtaka moja tu la kula njama za kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Denis Msacky. Kesi hiyo itatajwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger