Tuesday, May 21, 2013

"WAKRISTO MSIACHE KUSALI KWA KUOGOPA UGAIDI"....ASKOFU PENGO

Askofu wa Kanisa Katoliki,Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka waumini wa kanisa hilo kutoogopa kifo badala yake waendelee kwenda makanisani licha ya kuwapo kwa vitisho vya kushambuliwa.
Pengo alisema hayo jana katika Kanisa la Mtakatifu Joseph alipokuwa akitoa sakramenti ya kipaimara na aliwataka wasiwe na hofu lakini waendelee kumwamini Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu.
“Tuendelee kwenda makanisani,kamwe tusiogope kuuawa,tuwe na imani kwamba Yesu Kristo ndiye mlinzi wetu na ndiye atuongozaye,”alisema Pengo.
Kardinali Pengo alisema hata kama vyombo vya dola vitakuwa vimeshindwa kuwalinda,waumini kamwe wasiache kwenda makanisani kwa ajili ya kuabudu.
Pengo aliwataka waumini hao kutolipiza kisasi kutokana na mauaji yaliyotokea hivi karibuni mkoani Arusha kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya Yesu Kristo.
“Wakristo kulipa kisasi ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kikristo na sheria za nchi,” alionya Pengo.

Kauli hiyo imekuja baada ya watu watatu kuuawa kwa bomu na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa hivi karibuni katika Kanisa Katoliki,Parokia ya Joseph Mfanyakazi,Olasiti nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mauaji hayo yalitanguliwa na kuuawa kwa Padri Evarist Mushi aliyeuawa Februari 17 wakati akielekea katika Kanisa la Mtakatifu Theresia,Zanzibar kuendesha misa.
Pia Desemba 25 mwaka jana,Padri Ambrose Mkenda alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi watu wasiojulikana wakati akisubiri kufunguliwa geti nyumbani kwake Zanzibar.
Pengo aliwataka waumini wote kuendelea kusali kwa imani yao na kwamba matatizo yanayojitokeza yasiwakatishe tamaa.
Alisema hata katika mafundisho, kuna mambo mengi ambayo yalifanywa na baadhi ya watu ili kumkatisha tamaa Yesu Kristo asitimize malengo yake lakini baadaye alishinda.
“Vivyo hivyo waumini yanayojitokeza hivi sasa yasitukatishe tamaa tuendelee na utaratibu wetu wa siku zote na tutashinda,”alisema Pengo.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger