Tuesday, May 14, 2013

MFANYABIASHARA WA MADINI ANAYEDAIWA KUMUUA ASKARI APANDISHWA KIZIMBANI...!!

MFANYABIASHARA wa madini ya tanzanite, Lawi Abayo (33) amefikishwa kwenye Mahakama ya Mkoa wa Manyara akikabiliwa na mashitaka ya kumuua kwa kumpiga risasi askari polisi wa kituo cha Mirerani wilayani Simanjiro G.7037 Joseph Tairo (28).
Abayo alifikishwa mahakamani mjini Babati na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Rashid Chaungu. Mfanyabiashara huyo anatetewa na wakili maarufu wa kujitegemea wa jijini Arusha Duncan Oola.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi, Mbaruku Makame aliieleza Mahakama kuwa Abayo alitenda kosa hilo Aprili 7, mwaka huu kwenye Mtaa wa Kazamoyo katika Mji mdogo wa Mirerani.
Alidai kuwa Abayo alimpiga risasi ya kichwa askari wa Kituo cha Polisi, Mirerani wilayani Simanjiro, Tairo mkazi wa Kijiji cha Kabolo Mkuu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ambaye alifariki dunia Aprili 15, mwaka huu.
Aliongeza kuwa siku ya tukio hilo, Abayo bila halali alimpiga risasi askari huyo wakati akiwa kazini akimpeleka kwenye Kituo cha Polisi mhalifu aliyefanya vurugu kwenye Baa ya Kazamoyo Resort iliyopo mji mdogo wa Mirerani.
Makame alidai pia kuwa baada ya Tairo kumkamata mhalifu huyo, Abayo alikuja na gari aina ya Prado lenye namba za usajili T 671 ATK na kutoa bastola kisha kumpiga risasi ya kichwa na kuondoka na gari hilo akiwa na mhalifu huyo.
Mshtakiwa huyo Abayo hakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi hiyo na Hakimu Chaungu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 22, mwaka huu itakapotajwa tena.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

Habari Zinginezo:

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © 2025 GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger