Serikali
imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoagiza
transfoma nje ya nchi na badala yake kutumia zinazotengenezwa hapa
nchini na kampuni ya Tanalec.
Agizo
hilo limetolewa jana Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Tunduru Kusini, Mhe. Daimu Iddi Mpakate aliyetaka kujua ni lini Serikali
itatoa pesa kukamilisha miradi ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini
(REA).
Dkt.
Kalemani alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa ikilinganishwa na
mahitaji ya bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza
transforma hizo kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.
Kuhusu
suala la kugharamia nguzo kwa Mpango wa REA Dkt. Kalemani alisema mteja
hatakiwi kutozwa gharama yoyote ziadi ya Tshs. 27,000 fedha ya
kuunganishiwa umeme kwa mpango huu.Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali
inatekeleza Mradi wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi
hii inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016.
Alisema
Kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia
ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa Kilomita 293. 2, na ujenzi
wa njia nyingine yenye msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita
76.1 na ufungaji wa transfoma 38 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja
wa awali 3,330
“Gharama ya Mradi kwa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Wilaya ya Tunduru ni Tsh. Bilioni 32.56,” alisema Dkt Kalemani na kuongeza kuwa mkandarasi amekwishalipwa bilioni 27.22 sawa na asilimia 83.6 ya fedha.
Dkt.
Kalemani amesema kuwa katika Wilaya ya Tunduru ni vijiji vinne ambavyo
vimeunganishiwa miundombinu ya umeme na kufanyiwa majaribio kabla ya
kuwashiwa umeme.
Kwa
mujibu wa Dkt. Kalemani mkandarasi anaendelea kufunga transforma na
Mita za Luku katika vijiji 34 vilivyosalia kwa Wilaya ya Tunduru ili
viweze kupatiwa huduma ya umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
0 comments:
Post a Comment