Mchumi
na mtafiti wa uchumi amesema uamuzi wa Serikali kuipa Mamlaka ya Kodi
(TRA) kazi ya kukusanya kodi ya majengo badala ya halmashauri za wilaya,
utapunguza mapato hayo kutokana na upungufu wa rasilimali watu.
Akitoa
maoni yake kuhusu bajeti ya mwaka 2016/17 iliyowasilishwa bungeni juzi,
mchumi huyo, Simon Mapolu alisema TRA haitamudu kukusanya mapato hayo
kwa ufanisi kutokana na kuhitaji mtandao mpana wa watumishi kuweza
kufanya kazi zilizokuwa zikifanywa na halmashauri za wilaya, manispaa na
majiji.
“Halmashauri
za wilaya zina watumishi hadi ngazi ya mtaa kwa maana ya wenyeviti na
watendaji wa mitaa au vijiji ambao wanatumika kufuatilia na kukusanya
ushuru wa majengo, wakati TRA watumishi wao huishia ngazi ya wilaya na
maeneo machache kwenye vituo maalumu,” alisema Mapolu.
“Wakati
Sheria ya Kodi ya Mwaka 2004 inawafanya TRA kuwasubiria walipakodi
wawafuate ofisini, mamlaka za halmashauri huwafuata walipa kodi ya
majengo hukohuko waliko.”
Kuhusu
ongezeko la kodi kwenye vinywaji baridi na vikali, mchumi huyo alisema
ni kasumba inayolemaza wataalamu wa uchumi wa Serikali kufikiria
kuongeza kodi kwenye bidhaa hizo kila mwaka badala ya kubuni vyanzo
vipya.
“Kwa
mfano, kiwango cha kodi kilichoongezwa kwenye vileo na vinywaji baridi
kingekusanywa maradufu iwapo nguvu zaidi zingeelekezwa kwenye huduma za
simu, kama miamala ya fedha kwa njia ya mtandao,” alisema Mapolu.
Alisema
ukiacha miamala ya fedha, makampuni ya simu pia yanaingiza mamilioni ya
fedha kupitia gharama za miito ya simu na runinga kwa njia ya mtandao
ambayo haijakatwa kodi kwa kiwango kinachostahili.
“Kuna
zaidi ya Watanzania 30 milioni wenye kumiliki namba za simu, hawa
wakiweka muda wa maongezi ya Sh1, 000 kwa siku, makampuni hayo huingiza
zaidi ya Sh3 bilioni kwa siku bila kutozwa kodi stahiki,” alisema Mapolu
Kuhusu
Sh50 milioni zilizotengwa kwa kila kijiji kwa ajili ya mikopo kwa
wanawake na vijana, mtaalamu huyo alisema ni lengo jema, lakini akaonya
kuwa haiwezi kuleta tija iwapo hakutakuwa na mkakati thabiti na
unaoeleweka.
Alisema
fedha zilizotolewa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
na kubatizwa jina la “Mamilioni ya JK”, zilipotea kutokana na kutokuwepo
na mfumo wa kuzifuatilia.
0 comments:
Post a Comment