
Mbunge wa Konde Khatibu Said Haji (Cuf), jana aliibua sakata la Akaunti
ya Madeni ya Nje (EPA) bungeni akimtaja Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya
Kikwete kwamba alikiuka Katiba kwa kutoa msamaha kwa watu waliotuhumiwa.
Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk
Harrion Mwakyembe ilikanusha madai hayo na kusema Rais alikuwa sahihi
kwa kuwa viko vifungu ambavyo vinampa nafasi hiyo.
Katika swali
la nyongeza, mbunge huyo alihoji ni kwa nini Kikwete alitoa msamaha kwa
watu hao kabla hawajahukumiwa na Mahakama kama Katiba inavyosema.
“Kama
hivyo ndivyo, basi naomba ukubali kuwa Kikwete (Rais mstaafu) alivunja
Katiba ya nchi kwa kuwapa msamaha watuhumiwa wa EPA ambao walikuwa
hawajahukumiwa bado, naomba majibu,” alihoji Haji.
Katika swali
la msingi Mbunge huyo alitaka kujua iwapo Rais kwa mujibu wa Ibara ya 45
(1) A hadi D anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu
wa aina yoyote ambao mashauri yake yapo katika vyombo vya dola kwenye
hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani.
Waziri alisema ibara
hiyo ni kweli inampa mamlaka Rais ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote
aliyepatikana na hatia mbele ya Mahakama kupitia kifungu cha kwanza (1).
Dk Mwakyembe alisema kifungu (ii) kinampa Rais Mamlaka ya
kumwachia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa
kwa kosa lolote.
“Katika kifungu cha (iii) Rais anaweza
kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu kwa kosa lolote iwe adhabu
tahafifu na kifungu cha (iv) anaweza kufuta adhabu yoyote au sehemu ya
adhabu,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kwa kuzingatia masharti
ya Katiba, msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa
adhabu na Mahakama lakini watuhimiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako
hatua za upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya
ibara hiyo.
Alisema Rais hawezi kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa
uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola
kwani hatima ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka za
uchunguzi, mashtaka na Mahakama.
0 comments:
Post a Comment