Hapo zamani za kale palikuwepo na familia iliyojumuisha baba, mama na
mtoto mmoja wa kike. Mtoto huyo alikuwa mtundu sana na mara nyingi
alikuwa akiwaweka wazazi wake roho juu kutokana na michezo yake ya
kipuuzi.
Kila siku usiku muda wa kulala unapofika alikuwa na tabia ya kupiga
kelele kuwaambia wazazi wake kuwa chumbani kwake kuna joka kubwa
limeingia na linataka kummeza. Basi wazazi wake walipokuwa wakisikia
kelele hizo walikuwa wakikanyagana kuwahi chumbani kwa mtoto wao
kuangalia joka hilo na kumuokoa.
Kila walipokuwa wakifika walimkuta mtoto wao akicheka na kuwatania
wazazi wake ‘haoo waone walivyotoa macho, nilikuwa nawatania tu.’ Basi
wazazi walikaushia tu kwakuwa ndivyo walivyomlea mtoto wao na hawakuwa
tayari kumwadhibu.
Huo ndio ukawa mchezo wa mtoto huyo, kila siku ‘mamaa, babaa, joka
linataka kunimeza.’ Wazazi watakurupuka tena chumbani kwao kwenda
kumwangalia mtoto wao na kukuta hakuna nyoka wala nini! Wakati mwingine
walijikuta hata wakijeruhi vidole vyao vya miguu kwa kujigonga kwenye
samani za ndani wakiwahi kumsaidia binti yao. Mtoto huyo aliendelea
kuwafanyia vituko hivyo kwa muda na kwake ikawa ni burudani kweli kweli.
Siku moja, joka kubwa kweli liliingia ndani ya chumba cha huyo mtoto.
Alipiga kelele kama kawaida kuwaita wazazi wake waende kumuokoa. Wazazi
wakapuuzia kwasababu walijuwa kuwa ni yale yale, mtoto wao anawachezea
tu.
Mtoto alipiga kelele kuomba msaada asiupate hadi joka lile
likamvunjavunja, likammeza na kutokomea mwituni. Kulipokucha wazazi wake
walienda chumbani kumwangalia mtoto wao na kugundua ni kweli usiku
palikuja joka na kweli lilimmeza mtoto wao. Walilia na kuhuzunika sana.
HADITHI HII INA UHUSIANO GANI NA KIKI ZA KIBONGO?
Katika kutafuta kuongelewa zaidi kwenye TV, redio, blog na kwenye
mitandao ya kijamii, wasanii wetu wamekuwa wakitafuta njia nyingi
zikiwemo za kuunda matukio yasiyokuwepo. Mambo mengi sana ambayo
yamewahi kusemwa au kutendwa na wasanii yalikuja kugundulika kuwa kumbe
yalifanywa kwasababu ya kutafuta kiki tu.
Kwa mimi kama mwandishi, ninapoona kitu na kukikimbilia haraka
nikijua kuwa ni habari nzuri itakayowavutia wasomaji wangu na kuamua
kuiandika lakini baadaye nakuja kugundua haikuwa kweli, huwa nasosoneka
sana. Na mara nyingi hiyo hunifanya nipunguze kabisa imani na msanii
huyo.
Mashabiki pia hufedheheshwa na kiki hizi na wao pia hupunguza kabisa
imani na msanii. Matokeo yake, kama yule mtoto aliyewachosha wazazi wake
kwa kelele za kumezwa na nyoka ambaye hakuwepo na pindi nyoka wa kweli
anapomvamia wazazi wake wakapuuzia, ndivyo ambavyo wasanii wanaoendekeza
kiki hizi watajikuta wakishindwa kuaminiwa tena hata kwa matukio
makubwa ya kweli yatakayowahusu.
Wapo wasanii pia ambao wamekuwa na tabia za kuongea uongo uongo ili
waonekane wana mambo makubwa wanafanya. Wengine huamua kuishi maisha
‘feki’ kujitengenezea ukubwa ambao hawana.
Mara nyingi njia ya muongo ni fupi,
hujikuta wakiumbuka. Wengine pia huwindwa na maneno yao wenyewe ambayo
mwisho wa siku hugeuka kuwa jinamizi linalowatesa.
Acha kazi ziongee kwasababu ‘actions speak louder than words.’Ni vyema wasanii wakafikiria kabla ya kuamua kutengeneza kiki ambazo zitawatokea puani siku za usoni.
0 comments:
Post a Comment