ALIYEWAHI kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na
Waziri wa Mambo ya Nje, Ibrahim Kaduma amesema kasi ya Rais Dk.John
Magufuli inaweza kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisiwa na Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana alipozungumza na MTANZANIA
katika tamasha la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere kuhusu jinsi
viongozi wa sasa wanavyoendeleza misingi iliyoanzishwa Rais huyo wa
kwanza wa Tanzania.
Alisema tangu Nyerere aondoke madarakani suala la maadili ya uongozi
lilitetereka huku viongozi wakijinufaisha badala ya kuleta maendeleo
kwa wananchi wao.
“Tangu Mwalimu aondoke madarakani baadhi ya misingi ikiwamo ya
maadili na maendeleo ya watu imetetereka kwa kiasi kikubwa,” alisema na
kuongeza:
“Tunaweza kuwa na matumaini na Rais Magufuli kama ataendelea na kasi yake anaweza kuturudisha kule kwa Mwalimu Nyerere”.
Alisema Rais Magufuli ameanza kuonyesha njia ya kuelekea kusimamia maadili ya viongozi na kufungamanisha maendeleo na watu.
Ni vema rais aweke wazi dira yake na aijengee misingi ya sheria ili
kila mwananchi ajue serikali inataka kujenga nchi ya aina gani, alisema.
Awali akiwasilisha mada katika tamasha hilo iliyohusu “Mwalimu
Nyerere na Uongozi” Kaduma alisema uongozi kwa Mwalimu haukua fedha na
ufahari bali kujituma na kujitoa kwa ajili ya watu.
Kaduma alisema kiongozi anatakiwa asiwe mbinafsi bali awe tayari kuacha hata maslahi yake kwa ajili ya maslahi ya umma.
Dk. Bakari
Akizungumzia mpango wa serikali wa kugawa Sh milioni 50 kila kijiji,
aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo (TaSuBA) na mmoja wa
waliokuwa Mameneja wa vijiji vya ujamaa, Dk. Juma Bakari alisema mpango
huo unaweza usifanikiwe kutokana na kutokuwa na maandalizi mazuri.
Akieleza suala hilo kwa uzoefu wa vijiji vya ujamaa, alisema serikali
ya Mwalimu Nyerere haikuwa na maandalizi ya mpango ule ndiyo maana
haukufanikiwa na baadaye ukafa.
Suala la Sh milioni 50 kila kijiji halikuwa wazo la wananchi bali ni
wazo la mtu mmoja na hivyo linaweza lisitatue changamoto za watu wa
vijijini.
0 comments:
Post a Comment