WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wakuu wa nchini na washiriki wa
mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa wamevutiwa na jitihada
ambazo Tanzania imezichukua kukabiliana na janga hilo.
Ametoa
kauli hiyo leo (Ijumaa, Mei 13, 2016) wakati akitoa ufafanuzi kuhusu
ushiriki wake kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi ulioitishwa
kujadili suala la kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster
House, jijini London, Uingereza.
Waziri
Mkuu alisema katika kikao cha kwanza kilichohudhuriwa na wakuu wa nchi
na viongozi wa kitaifa wapatao 20, alipata fursa ya kuelezea jinsi
Tanzania ilivyoweza kupambana na rushwa kwa kuzingatia vigezo vikuu
vinne.
Waziri
Mkuu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni kufanya marekebisho ya baadhi ya
sheria zinazohusu masuala ya rushwa; uanzishwaji wa mahakama maalum ya
mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi Julai, mwaka huu; mikakati ya
udhibiti wa fedha za miradi ya wananchi na utaratibu wa kubaini wala
rushwa kwa kushirikisha jamii ikiwemo kutunza siri za watoa taarifa.
“Ziko
sheria ambazo zinafanyiwa kazi hivi sasa ambazo ni lazima zipitishwe na
Baraza la Mawaziri kabla mahakama hii haijaanzishwa, zikishapitishwa na
Baraza ndipo zitaanza kutumika,” alisema.
Akifafanua
kuhusu mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya maendeleo, Waziri
Mkuu alisema kwamba katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imeweza
kuongeza kiasi cha fedha zilizotengwa kwa shughuli za maendeleo kutoka
asilimia 27 hadi kufikia asilimia 40.
“Kuongezeka
kwa kiwango hiki ni ishara tosha kuwa tumelenga kutoa huduma kwa
Watanzania na muhimu katika rushwa ni udhibiti wa fedha hizo na
kuhakikisha zinakwenda kwenye miradi; matuizi mazuri ya fedha za
Serikali, matumizi mazuri ya fedha zinazochangiwa na wahisani ili ziweze
kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” alisema.
“Tumekubaliana
na uwepo wa uwazi na kushirikishana taarifa hasa katika kupeana taarifa
za makampuni yanayoanzishwa na kusajiliwa katika nchi zinazoendelea
kama njia ya kudhibiti tabia ya nchi ndogo kama Ireland na Panama
kupokea na kuficha fedha zinazotoka kwenye nchi zinazoendelea” alisema.
Alisema
kila nchi imesisitizwa kutumia raia na kuwalinda watoa siri, kutumia
mifumo ya kiintelijensia, kutumia wanasheria na kuchukua hatua
mbalimbali dhidi ya watu wanaokamatwa kwa masuala ya rushwa.
Waziri
Mkuu alisema alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw.
David Cameron ambaye mbali na kupongeza juhudi za Serikali ya Rais Dk.
John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa pia aliahidi kutoa
mwaliko ili Tanzania iweze kushiriki kwenye mkutano mwingine wa masuala
ya rushwa utakaofanyika Japan, Julai mwaka huu.
“Anataka
Tanzania iende kwenye mkutano huo ili ikaelezee mafanikio iliyoyapata
katika kukabili suala hili, ili pia nchi nyingine ziweze kuiga utaratibu
ambao Serikali imeutumia hadi tukafanikiwa katika mapambano dhidi ya
rushwa,” alisema Waziri Mkuu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ofisi yake haijahusika na
kuandaa mkutano wa wanadiaspora waishio Uingereza kama ambavyo imedaiwa
na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna watu maalum
wamechaguliwa kushiriki mkutano huo.
Amesema
mkutano huo umepangwa kufanyika kesho (Jumamosi, Mei 14, 2016) na uko
wazi kwa Watanzania wote kushiriki ili waje kusikiliza nchi yao imefanya
nini na kama kuna masuala yanahitaji ufafanuzi, watapatiwa fursa hiyo.
“Kulikuwa
na hofu ya watu wanaotoka mbali kutoweza kushiriki sababu ya gharama,
lakini nasema yeyote mwenye uwezo wa kuja aje ndiyo maana tumeuweka muda
wa asubuhi ili watu waweze kushiriki na kuwahi kurudi makwao,” alisema.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, MEI 13, 2016.
0 comments:
Post a Comment