Ndani
ya miezi sita tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanikiwa
kuokoa asilimia nne ya bajeti yake ya kwanza katika hatua alizochukua
katika kubana matumizi na kudhibiti ufisadi.
Rais
Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka jana alianza kwa kusisitiza
kubana matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka
vyanzo mbalimbali, jambo alilolifanikisha kulingana na ripoti za kila
mwezi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
TRA
ilitangaza kukusanya Sh1.4 trilioni Desemba mwaka jana, Januari
ikakusanya Sh1.08 trilioni na Sh1.04 trilioni Februari kabla
haijakusanya Sh1.316 triioni mwezi Machi.
Makusanyo
hayo yote yalikuwa ni zaidi ya matarajio. Licha ya mapato hayo
yaliyokusanywa kwa taratibu za mamlaka hiyo, Rais Magufuli amefanikiwa
kuokoa zaidi ya Sh1.02 trilioni ndani ya muda aliokaa madarakani.
Serikali
imependekeza bajeti ya Sh29.5 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha. Akisoma
makadirio ya mapato na matumizi hayo kwenye kamati za Bunge, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Sh17.7 trilioni zitakuwa ni
za matumizi ya kawaida na Sh11.8 trilioni kwa ajili ya miradi ya
maendeleo.
Kiasi
kilichookolewa na Rais Magufuli ni takribani nusu ya mapato
yatakayotokana na vyanzo visivyo vya kodi na pia zaidi ya mara mbili ya
mapato yatakayokusanywa na halmashauri zote nchini kwa kipindi hicho.
Ni
fedha nyingi zikilinganishwa na zile zilotolewa na Shirika la Msaada la
Marekani (MCC) awamu ya kwanza kutekeleza usambazaji wa umeme vijijini.
Ndani ya siku 30 za kwanza; baada ya kufanya safari ya kushtukiza
hazina na kutembelea bandarini mara kadhaa aliokoa takribani Sh1
trilioni.
Makontena
zaidi ya 2,500 yaliyobainika kuondoshwa bila kulipiwa ushuru na tozo
nyinginezo yaliipa Serikali Sh637.2 bilioni. Fedha hizo zilitokana na
malipo ya lazima pamoja na faini kwa wakwepaji.
Bado
Novemba mwaka jana wakati anazindua Bunge, Rais alikataa kufanya
sherehe zilizoandaliwa na wabunge na akaagiza Sh225 milioni zielekezwe
kwenye maeneo yenye uhitaji. Maamuzi hayo yalizipeleka fedha hizo
kununua vitanda 300, magodoro 300, mablanketi 1,675 na viti vya
magurudumu 30 ambavyo vilikabidhiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH).
Kwenye
mkutano huo, Rais aliliambia Bunge kuwa hatua yake ya kuzuia safari za
nje kwa watumishi wa umma imeokoa Sh356.3 bilioni ambazo zinaweza
kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.
Desemba
9, mwaka jana, Dk Magufuli aliahirisha sherehe za uhuru na akaagiza Sh4
bilioni zilizotengwa zitumike kupanua barabara kutoka Morocco mpaka
Mwenge, jijini hapa. Utekelezaji wa agizo hilo unaendelea.
Muda
mfupi baada ya kuteua mawaziri na manaibu wao, alifuta semina elekezi
kwa viongozi hao. Hapa aliokoa Sh2 bilioni ambazo zilipangiwa matumizi
mengine.
Mapema
Aprili alifuta sherehe za Maadhimisho ya Muungano na kuelekeza Sh2
bilioni zilizotengwa kwa ajili hiyo zitumike kupanua barabara ya Uwanja
wa Ndege-Mwanza.
Katika
kile kilichoonekana kuwa ni kuunga mkono juhudi za kubana matumizi,
Bunge liliokoa Sh6 bilioni ambazo ilizikabidhi kwa Rais ili zinunue
madawati kwa shule zenye upungufu nchini
0 comments:
Post a Comment