Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaja mambo
manne ambayo ni vikwazo ndani ya sekta ya sanaa ya filamu nchini na
kuyaita kwamba ni majipu huku akisisitiza kwamba Serikali itatunga sera
ya sekta hiyo katika mwaka wa fedha 2016/17.
Nape aliyataja mambo hayo na kuyafananisha na majipu kuwa ni uporaji
wa kazi za wasanii nchini, ujenzi duni wa miundombinu ya kazi za
wasanii, usimamizi mbovu wa Bodi ya Filamu, sanjari na tatizo la mfumo
mbovu wa usambazaji wa kazi za wasanii.
Akizungumza wakati akizindua tamasha la filamu la Tanzanite
International Film Festival (TIFF) jijini Arusha juzi ambalo
lilihudhuriwa na wasanii maarufu wa filamu nchini, waziri huyo alisema
kwamba jipu la kwanza ambalo atakwenda kulitumbua ni uporaji wa kazi za
wasanii nchini.
Hata hivyo, alisema kwamba jipu la pili ni ujenzi duni wa miundombinu
ya kazi za wasanii za filamu na kudai kwamba chini ya uongozi wake
atahakikisha anaimarisha miundombinu bora kwa lengo la kuwasaidia
wasanii hao pamoja na kulinda haki zao.
Alisema ya kwamba mfumo wa kazi za usambazaji wa kazi za wasanii
nchini pamoja na hakimiliki ni wa kinyonyaji huku akitolea mfano wa kazi
za msanii maarufu wa sanaa hiyo nchini, Steven Kanumba na kusema kwamba
familia yake hainufaiki na matunda ya kazi zake hadi sasa kutokana na
mfumo mbovu wa usimamizi wa kazi za wasanii.
Alitaja takwimu kwamba
mwaka 2011/12, filamu 218 zilitengenezwa nchini na mwaka 2014/15 kazi
hizo ziliongezeka hadi kufikia 1,400.
0 comments:
Post a Comment