MAWAZIRI
wa Serikali ya Awamu ya Tano wamewajia juu wabunge wa upinzani na
wananchi wanaovishutumu kila mara vyombo vya ulinzi nchini na kuwataka
kuacha kuvihusisha vyombo hivyo na masuala ya kisiasa.
Mawaziri
hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January
Makamba.
Wamewataka
wananchi na hususani wabunge wa vyama vya upinzani, kutambua kuwa
vyombo hivyo vya ulinzi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na Polisi wajibu wake mkubwa ni kulinda mipaka ya
nchi na usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza
wakati wa mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara inayoshughulikia Muungano na Mazingira, Dk Mwinyi alisema
haijawahi kutokea na wala haitotokea jeshi kutumika kisiasa.
Alisema
Jeshi la Tanzania limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa kufuata
sheria iliyojiwekea pamoja na za kimataifa na wala hata siku moja
haliwezi kutumika kwa ajili ya kutumiza malengo ya kundi fulani.
“Jeshi
letu lina sifa ya kimataifa ya ulinzi wa amani, dunia kote tunasifika
kwa weledi, kulinda amani na mipaka yetu. Haijawahi kutokea wala
haitotokea jeshi kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa,” alisisitiza Dk Mwinyi.
Alisema
tangu mjadala wa makadirio ya bajeti hiyo uanze, baadhi ya wabunge
hususani wabunge wa upinzani wamekuwa wakilitupia shutuma nzito jeshi na
vyombo vya dola kwa ujumla kuwa limetumika vibaya kwenye uchaguzi wa
Zanzibar na chaguzi nyingine.
Aliwataka
wabunge hao pamoja na wananchi wanaovilaumu mara kwa mara vyombo hivyo
vya dola kumuogopa Mungu kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya vyombo vyao
vya ulinzi na usalama.
Alisema
madai kuwa jeshi hilo limetumika na kuandikisha wananchi kwenye kambi
zao za jeshi visiwani Zanzibar si ya kweli na kama kuna mwenye ushahidi
auwasilishe ili ukweli ujulikane.
Dk
Mwinyi alisema amesikitishwa na madai ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani
kuhusu masuala ya Muungano, Ally Abdallah Saleh kwamba Zanzibar imetekwa
na jeshi la Tanganyika kana kwamba nchi iko katika vita.
“Naomba
nikujibu kwanza ili ufahamu kuwa hakuna jeshi la Tanganyika, jeshi ni
moja na ni la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Naomba nimuelimishe kazi
kubwa za jeshi ni ulinzi wa mipaka, ulinzi wa amani na kutoa msaada kwa
mamlaka za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama inapohitajika
kufanya hivyo,” alisema.
Alisema
inapotokea matukio makubwa kama shughuli ya uchaguzi, duniani kote si
Tanzania pekee, majeshi yote yanakuwa tayari kukabiliana na hali yoyote
na ndio maana askari wake wanakuwa kwenye sare za kombati.
Kuhusu
madai ya kambi hiyo ya upinzani kuwa Jeshi limekuwa likitumika
kulazimisha Muungano, Dk Mwinyi alisema JWTZ ni kielelezo cha Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema
tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane mwaka 1964, jeshi ni moja na
kamwe halijawahi kulazimisha utawala, ila lipo hadi Zanzibar kwa sababu
ya kulinda mipaka ya Tanzania, na Zanzibar ni sehemu ya Tanzania.
“Tangu
mwaka 1964 jeshi lina vikosi vyake Zanzibar na siku zote vikosi hivi
huwa na silaha, sasa tuna haja gani ya kupeleka wanajeshi na silaha
wakati miaka yote vyote viko huko? "Alihoji Dk Mwinyi.
Naye Naibu Waziri Masauni alisema hoja kwamba jeshi lilitumia mabavu Zanzibar na askari walikuwa ni wengi si ya kweli.
Naye Naibu Waziri Masauni alisema hoja kwamba jeshi lilitumia mabavu Zanzibar na askari walikuwa ni wengi si ya kweli.
Alisema
kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, kila kituo cha uchaguzi
kinahitajika angalau askari wawili wakati Zanzibar kulikuwa na vituo vya
uchaguzi zaidi ya 3,000 na askari waliopo visiwani humo ni 5,000.
Alisema
kwa hali ilivyokuwa askari wa Zanzibar walikuwa hawatoshi kwani
wangesambazwa wote wasingetosha kuweka ulinzi na kuhakikisha uchaguzi
unafanyika kwa utulivu na usalama.
Kuhusu
madai kwamba Katiba imekiukwa, aliutaka upande wa upinzani kujiuliza
kati ya madai yao ya kumtaka Rais John Magufuli aingilie mamlaka ya Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) au Polisi kulinda raia na mali zao, kipi ni
uvunjifu wa Katiba.
Alifafanua
kuwa majukumu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni
kulinda usalama wa raia na mali zao hivyo bila kujali cheo au utajiri
wa mtu yeyote endapo atavunja sheria atachukuliwa hatua za kisheria.
Naye
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alisema uchaguzi wa
Zanzibar ulikamilika kwa usalama na kwamba pamoja na malalamiko ya
vichochoroni kuhusu uchaguzi huo, hakuna hata mmoja aliyefungua kesi
kupinga matokeo mahakamani.
Alisema
kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ni ruhusa mtu asiporidhika na matokeo
ya uchaguzi, kufungua kesi ya kuyapinga, lakini tangu uchaguzi huo
umalizike hakuna mtu kutoka jimbo lolote visiwani humo aliyefungua kesi.
Naye
January alisema kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, Mahakama Kuu ya Zanzibar
ndio pekee yenye uwezo wa kusikiliza na kuamua masuala yote yanayohusu
uchaguzi wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment