Wakati
Serikali ya Awamu ya Tano ikizuia maofisa na watumishi wa umma kwenda
nje ya nchi kwa safari ambazo si za lazima ili kubana matumizi, Bunge
limesema limetenga fungu kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kupata mafunzo
ya uendeshaji bora wa Bunge nje ya nchi.
Novemba
7, mwaka jana, ikiwa ni siku mbili tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa
Tano, John Magufuli alipiga marufuku safari za nje kwa maofisa wa
serikali isipokuwa tu itakapokuwa lazima na kwa ruhusa ya Ikulu.
Rais
Magufuli alisema shughuli nyingi za nje ya nchi zitafanywa na
kusimamiwa na mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi hizo.
Wakati
Rais Magufuli akitekeleza sera yake ya 'Hapa Kazi Tu' kwa kubana
matumizi kiasi cha kuzuia semina elekezi kwa mawaziri ambayo ingeharimu
Sh. bilioni mbili, uongozi wa Bunge jana ulisema umepanga kupeleka
wabunge ughaibuni kwa ajili ya mafunzo.
Akifungua
semina ya wenyeviti wa kamati za Bunge iliyofanyika mjini hapa juzi,
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema uongozi wa Bunge hilo utaandaa
mafunzo kwa vitendo nje ya nchi kwa ajili ya wabunge.
"Katika
siku za usoni, pia tutaandaa mafunzo haya kwa vitendo nje ya nchi. Lipo
Bunge moja tu Tanzania; na hivyo mafunzo pekee ya vitendo ni kwa
kutembelea mabunge ya wenzetu," alisema Ndugai na kuibuka shangwe za wenyeviti wa kamati za Bunge ukumbini.
Baadhi yao walimuomba arudie kuelezea dhamira hiyo. "Nafurahi kwamba tuna mawasiliano mazuri na mabunge mengi ya nchi zinazoendelea kama vile Uingereza, India na hata Marekani," alisema Ndugai ambaye Bunge lake, kwa vyovyote, limeathiriwa na mkakati wa serikali wa kubana matumizi.
"Lakini
pia kwa majirani zetu hapa, yaani Zambia, Kenya, Uganda, Afrika Kusini
na kadhalika. Tutatumia ujirani na uhusiano wetu na mabunge hayo ili
mfaidike kwa mafunzo."
Baada
ya kufungua rasmi mafunzo hayo, Ndugai alisema kuwa wameona kuna
ulazima wa kuwa na mafunzo kwa wabunge ndani na nje ya nchi kutokana na
wengi wao kuwa wageni wa uendeshaji wa Bunge.
"Kazi ni kubwa sana (kuedesha shughuli za Bunge). Ni kama tunaanza upya kwa sababu wabunge wengi ni wapya," alisema.
"Tumeamua kuwa na mafunzo haya ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuwa na uendeshaji bora wa bunge."
Ndugai
alisema kutakuwa na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi mbalimbali
yakiwamo ya wabunge wote, wanawake, vijana, viongozi wa wabunge na
kamati za Bunge.
Aliongeza
kuwa tayari kuna fungu ambalo limetengwa kwa ajili ya kugharamia
mafunzo hayo, lakini hakuwa tayari kuanika kiasi cha fedha
kilichotengwa, hata hivyo.Alipoulizwa kuhusu kukinzana na agizo la Rais
Magufuli, Spika huyo alisema:
"Ni
kweli kwamba alichosema Mheshimiwa Rais cha kupunguza safari za nje.
Sisi (Bunge) pia tumejitahidi sana kupunguza safari za nje, lakini
katika mafunzo haya, inafikia wakati mtu lazima aone Bunge jingine
linafanya nini.
"Wajue nao wenzao duniani wanafanya nini. Ila wasiwe wengi na haitakuwa mara kwa mara."
Ndugai pia alilimwagia sifa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) kwa kufadhili mafunzo ya wabunge, ikiwamo semina ya jana, kupitia
mradi wa wake wa kusaidia mabunge (LSP).
Alisema
mradi huo umekuwa ukisaidia kutoa semina kwa kamati mbalimbali za Bunge
ili kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo katika kutekeleza majukumu
yao ya kikatiba kwa ufanisi zaidi.
Alisema
mradi huo ulioanza rasmi 2011, utamalizika mwezi ujao, lakini
mazungumzo yanaendelea ili uendelee hadi 2020 na kwamba wafadhili
wameonyesha nia ya kuendelea katika Bunge la 11 kuanzia Julai, mwaka huu
hadi Juni, 2020.
Katika
semina ya jana ambayo Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alishiriki,
kulikuwa na mafunzo ya mchakato wa kutunga sheria na uchambuzi wa
miswada, mchakato wa maandalizi ya Bajeti ya Serikali na Sheria ya
Bajeti ya mwaka 2015 pamoja na majukumu wenyeviti wa kamati za Bunge na
namna ya kuzungumza mbele ya hadhara.
Semina
hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Kamishna wa Bajeti - Mikoa na
Halmashauri, Dk. Charles Mwamwaja na mawakili Said Yakubu na Harold
Sungusia waliokuwa watoa mada, kulikuwa na mafunzo ya namna ya kutumia
vyombo vya habari wakati wa shughuli za kamati na mabadiliko, maboresho
na hatma ya Bunge.
Masharti
Mwishoni
mwa mwaka jana, Ofisi ya Rais ilisambaza mwongozo kwa taasisi na
mashirika ya umma unaoweka masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka
kusafiri nje ya nchi watatakiwa kuyatimiza ili wapewe kibali cha
kusafiri.
Masharti
hayo ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi na maombi hayo
yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda Ikulu ili mwombaji
aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa safari hiyo na tija
itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Masharti
hayo yanamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama taasisi kama Bunge, apime
kama safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi
kabla ya kuwasilishwa Hazina.
Sharti
lingine ni kupima umuhimu wa safari hiyo na kuona isipofanyika
itaathiri vipi taifa, na mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa
taasisi na taifa kama imewahi kufanyika huko nyuma.
Ofisi
za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina Novemba 12, mwaka
jana zikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla kwa safari za nje
ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake.
Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale itakavyoelekezwa vinginevyo.
Akihutubia
katika ufunguzi wa Bunge la 11 Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli
alisema safari za nje katika mwaka mmoja na nusu wa mwisho ya awamu ya
nne zilitafuna zaidi ya Sh. bilioni 4, kiasi ambacho kingeweza kujenga
kilometa 40 za barabara ya lami
0 comments:
Post a Comment