Tuesday, May 3, 2016

Afungwa Miaka Mitatu Kwa Kuiibia Benki ya Wanawake zaidi ya milioni 10

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imemuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, Nicolaus Mdehwa (27) baada ya kupatikana na hatia ya kuiba Sh 11.9 milioni mali ya Benki ya Wanawake Tanzania (TWB).

Mshtakiwa huyo pia ametakiwa na mahakama hiyo kulipa fidia ya Sh 11.9 milioni alizoiba.
Mdehwa ambaye ni mfanyabiashara wa matunda na mkazi wa Kigamboni-Tungi Standi, anadaiwa kuiba kiasi hicho cha fedha kupitia mashine ya kutolea fedha (ATM) ya Umoja iliyopo Makao makuu ya Benki ya Afrika (BOA) maeneo ya mtaa wa Ohio wakati akijua kuwa mashine hiyo ilikuwa ina tatizo.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Adolf Sachore amesema mahakama yake imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne.
“Upande wa mashtaka ulileta mashahidi wanne kuthibitisha shtaka hili na hivyo mahakama kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh 11.9 milioni”amesema hakimu Sachore.
Amesema kupitia mashahidi hao, wameithibitishia mahakama hiyo kwamba mshitakiwa alikuwa ni mteja katika Benki ya Wanawake Tanzania akitumia akaunti namba 300068961.
Aliendelea kueleza kuwa mshitakiwa huyo alitumia Mashine ya kutolea fedha (ATM) ya Umoja iliyopo Benki ya Afrika (BOA) maeneo ya mtaa wa Ohio huku akijua kwamba mashine hiyo ina tatizo.
‘’Katika ushahidi uliotolewa mahakamani, mashahidi walidai kuwa mshitakiwa alitumia ATM hiyo ambayo ilikuwa ina matatizo kutoa Sh 11.9milioni wakati akijua wazi kuwa akaunti yake ilikuwa na Sh 260,000 pekee,’’ amesema Hakimu Sachore.
Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe kuwa fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za wizi kama za mshtakiwa.
“Naiomba mahakama hii itoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa vijana wengine ambao wanatumia njia ya mkato kujipatia fedha”alidai wakili Mwenda.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwanini asipewe adhabu, hata hivyo Mdehwa alijitetea kwa kuiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni kosa lake la kwanza.
Awali akisoma hati ya mashtaka, wakili Mwenda alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Mei 20, 2010 na Juni 17, mwaka huo huo, katikati ya jiji la Dar es Salaam katika Benki ya Wanawake Tanzania (TWB).
Ilidaiwa katika tarehe hizo mshtakiwa aliiba Sh 11.9milioni mali ya TWB huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger