SERIKALI imeingilia kati mpango wa Mbunge wa Meatu, Salum Khamis
‘Mbuzi’ (CCM) wa kutaka kuchimba madini ndani ya pori la hifadhi na
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika eneo la Makao (JUHIWAPOMA)
wilayani Meatu.
Eneo la Makao linaendeshwa kisheria na Kampuni ya Mwiba Holdings Limited.
Mbunge huyo pamoja na washirika wake, Enock Yakobo na Abdillahi
Lessani, walipewa leseni Novemba 18,2014 iliyosainiwa na Ofisa Madini
Kanda ya Ziwa, Juma Semanta. Leseni hiyo itadumu kwa miaka
saba.
Hata hivyo, Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, imeunda kikosi
kazi kuchunguza uhalali wa leseni hiyo ambayo inadaiwa imetolewa kwa
‘mlango wa nyuma’.
Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa baada ya kukamilika
ripoti hiyo ya uchunguzi ikiwamo kubaini watumishi waliohusika kutoa
leseni hiyo, suala hilo litakabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
kesho mjini Dodoma.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Makao wilayani Meatu
juzi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alitangaza kusimamishwa
mpango wa uchumbaji madini katika eneo hilo kuepusha mgogoro wa
masilahi katika eneo hilo.
“Tunasimamisha huu mpango wa kuchimba madini. Kinachowa gombanisha
hapa ni uamuzi ambao ninyi mliufanya huko nyuma. Leo (juzi), mnasema
hamna eneo la kuchunga mifugo. Kwa hiyo habari ya madini hapana,”
alisema Mtaka.
RC pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, Godfrey
Machumu, kuhakikisha Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makao, Isack Magaka,
anakamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Polisi kwa kukwepa kuhudhuria
mkutano huo wa kujadili mgogoro uliopo.
Mtaka alitoa agizo hilo baada ya kutaka Magaka ajitokeze kuwaeleza
wanakijiji taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazotolewa na
kampuni ya Mwiba, ndipo ilipobainika kwamba hakuwapo mkutanoni hapo.
“Lazima tuhoji matumizi ya fedha za wananchi,” alisema Mtaka.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, Anthony Philip, alikiri mbele
ya mkutano huo kuwa kijiji hicho kimekuwa kikipokea Sh milioni 115 ,
zikiwamo Sh milioni 80 za kodi ya pango kila mwaka kutoka kampuni ya
Mwiba yenye mkataba wa kuendesha shughuli za uwindaji wa utalii na
upigaji picha katika pori hilo.
Mbali ya fedha hizo, Meneja Uhusiano wa Mwiba Holdings Limited,
Clarence Msafiri, alisema kampuni hiyo pia imekuwa ikikipatia kijiji
hicho Sh milioni mbili kila mwaka kwa ajili ya kodi ya uwanja wa ndege
na fedha nyingine nje ya makubaliano kwa ajili ya kuchangia
utekelezaji wa miradi ya jamii kijijini hapo.
“Tunalipa Sh milioni mbili kila mwaka kwa ajili ya uwanja wa ndege na
tunatoa fedha nyingine zisizo kwenye makubaliano yetu (Mwiba) na kijiji
cha Makao kuchangia maendeleo.
“Mfano hivi sasa tumejipanga kuchangia ununuzi wa madawati kwa
ajili ya wanafunzi shuleni kuitikia wito wa Rais John Magufuli,” alisema
Msafiri.
Kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Kijiji cha Makao na kampuni ya
Mwiba, Mtaka alimtaka mwenyekiti wa kijiji kwa niaba ya wanakijiji
kutangaza kusudio la mgogoro na kampuni hiyo ili liwekwe kwenye
maandishi na hatimaye Serikali ilitafutie usuluhishi wa sheria.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, tumesikiliza tuhuma dhidi ya
Mwiba. Kwa kuwa jambo hili ni la sheria, sheria inamtaka mwenyekiti wa
kijiji atangaze kusudio la mgogoro na kampuni ya Mwiba ili liwekwe
kwenye maandishi kwa ajili ya kutafutiwa usuluhishi kukiepushia kijiji
hiki matatizo,” alisema Mtaka.
Mwenyekiti wa Kijiji, Philip, alipewa nafasi mkutanoni na kusema,
“Mimi naomba tu ndugu zangu wananchi kwamba ninatangaza kusudio la
mgogoro na kampuni ya Mwiba.”
Mgogoro baina ya pande hizo mbili unadaiwa kuikwamisha kampuni ya
Mwiba kukabidhi Sh milioni 356 ilizotenga mwaka huu kwa ajili ya
kuchangia gharama za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vijiji
vya Makao, Iramba Ndogo, Mwangudo, Sapa, Mbushi, Jinamo na Mwabagimu
vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika eneo hilo.
Profesa Maghembe
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe, aliomba Watanzania wawe na subira katika suala hilo
kwa vile Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anton Mtaka, analishughulikia kwa
uzito na taarifa yake ataiwasilisha serikalini kesho.
“Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori inaeleza wazi kuwa hakuna umiliki katika eneo la juu ya ardhi ambayo ni hifadhi.
“Hata waliotoa leseni ya uchimbaji wa madini kuna shaka ndani yake ila naamini taarifa ya Mkoa wa Simiyu itaeleza kwa kina.
“Hivi sasa tunajua kuna watu kazi yao ni kutaka kukwamisha juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambaye
amedhamiria kuijenga Tanzania ya viwanda.
“Wao wamekuwa na kazi ya kueneza kila aina ya uchafu na uongo kwa
wawekezaji ambao wana nia njema, hawa tutawashughulikia tu,” alisema
Profesa Maghembe.
Mbunge wa Meatu, Salum Khamis alipotafutwa kupata
ufafanuzi wa madai hayo dhidi yake, simu yake haikupatikana hadi
tunakwenda mtamboni.
0 comments:
Post a Comment