RAIS Dk. John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551, huku
akiwanyima msamaha kwa mara ya kwanza wezi wa pikipiki, maarufu kama
bodaboda na magari.
Kati ya wafungwa hao 3,551, Rais Magufuli amewaachia huru 580 na wengine 2,971 wamepunguzia moja ya sita ya vifungo vyao.
Rais alitoa msamaha huo jana wakati wa maazimisho ya miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na
kusainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali
mstaafu Projest Rwegasira, ilisema wezi wa pikipiki na magari ni
miongoni mwa waliokosa msamaha kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
“Rais kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa msamaha kwa wafungwa
3,551 ambapo 2,971 watapunguziwa vifungo vyao kwa asilimia moja ya sita
na 580 kuwachiwa huru,” ilisema taarifa hiyo.
Rais Magufuli alisema ni mategemeo ya Serikali kuwa wafungwa
watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wenzao kujenga
Taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Wafungwa walionufaika na msamaha huo, ni wale wenye ugonjwa kama
Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wamethibitishwa na jopo la waganga
chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Wilaya.
“Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike
walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na
wasionyonya.
“Wengine walionufaika na msamaha ni wenye ulemavu wa mwili na akili
ambao ulemavu huo umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti
wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Mganga Mkuu wa Wilaya,” ilisema taarifa hiyo.
Wafungwa ambao hawakuguswa na msamaha huo, ni wale waliohukumiwa
kunyongwa, waliopewa adhabu ya kunyongwa na kubadilishwa kuwa kifungo
cha maisha au kifungo gerezani.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na
matumizi ya dawa za kulevya (cocaine, heroin na bhangi), makosa ya
rushwa, makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au
kujaribu kutenda makosa hayo.
Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha,
risasi au milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi,
kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
Rais pia hakuwasamehe wanaotumikia kifungo kwa kuwapa mimba wanafunzi
wa shule za msingi na sekondari na ambao walitenda makosa hayo wakiwa
na umri wa miaka 18, wale wenye makosa ya wizi wa magari na pikipiki,
wanaotumikia kifungo chini ya sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya
Huduma kwa Jamii.
“Waliokosa msamaha wengine ni wale waliotumia vibaya madaraka,
waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na bado wangali
wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
“Wafungwa waliozuia watoto kupata masomo, wenye makosa ya utekaji wa
watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya
binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu
wenye ualbino,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, Rais Magufuli hakuwasamehe waliofungwa kwa makosa ya
usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, wizi ama ubadhirifu wa
fedha za Serikali, makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini
ya ulinzi halali na wafungwa walioingia gerezani baada ya Februari 26
mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment