Thursday, November 19, 2015

Dr.Tulia:Sijapandikizwa ili Niibebe Serikali

Mgombea unaibu spika kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Tulia Ackson Mwansasu, amekanusha madai kwamba amepewa nafasi hiyo kama pandikizi ili aibebe Serikali.

Amesema madai kuwa ataibeba Serikali kwa kuwa ni mbunge wa kuteuliwa hayana msingi kwa kuwa haendi bungeni kumtumikia rais bali kuwatumikia Watanzania.

Rais John Magufuli Jumatatu wiki hii alimteua Dk. Ackson kuwa mbunge wa kuteuliwa na kutengua nafasi yake ya naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali aliyoteuliwa hivi karibuni na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

“Ni kweli nimeteuliwa na rais, lakini nakwenda kufanya kazi za Watanzania, nikipata nafasi ya kuwa naibu Spika madai kuwa nitaibeba serikali hayapo kwa kuwa nitafanya kazi za Bunge ambazo ni kuisimamia, kuishauri na kuiwajibisha serikali,” alisema Dk. Ackson ambaye juzi usiku alipitishwa kwa kauli moja na wabunge wa CCM kuwa mgombea wake wa unaibu spika.

Alisema ni vyema wabunge wakawa na imani naye na kumpa ushirikiano wa dhati ili atekeleze majukumu yake ipasavyo.
Katika hatua nyingine, vita ya unaibu Spika wa Bunge la 11, imemalizika, baada ya, Dk. Ackson, kupitishwa kwa kauli moja na wabunge wa CCM kugombea nafasi hiyo.

Awali kulikuwa na mvutano wa ndani kwa ndani baina ya wabunge wa chama hicho, ambao waligawanyika kwa baadhi kumtaka Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

Habari Zinginezo:

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © 2025 GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger