Uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia Biometric Voters
Registration (BVR) Dar es Salaam, unaanza rasmi kesho, huku mashine
zaidi ya 4,000 zikitarajia kutumika kukamilisha kazi hiyo katika vituo
1,700.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema tume ina imani uandikishaji
utafanyika kwa utulivu na amani.
“Mkoa wa Dar es Salaam umepata bahati, kwani tunatarajia kuwa na vifaa vya kutosha,” alisema Lubuva na kuongeza:
“Kuna
vifaa vingi vinarejeshwa kutoka mikoani, tunatarajia vitatumika vizuri
hapa.” Alisema NEC tayari imekutana na wadau wakiwamo viongozi wa ngazi
mbalimbali na kuwataka kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha.
Kwa
mujibu wa takwimu za Shirika la Takwimu la Taifa (NBS) za makadirio ya
watu wenye sifa ya kupiga kura, zinaonyesha kuwa Dar es Salaam ina zaidi
ya watu milioni 2.9, idadi ambayo ni sawa na jumla ya wapigakura katika
mikoa sita ya Katavi, Lindi, Shinyanga, Njombe, Iringa na Rukwa.
Awali,
NEC ilitangaza kuahirishwa tarehe ya kuanza uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hadi hapo
itakapotangaza tena.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba alisema hatua hiyo ilitokana na kuchelewa kuwasili kwa vifaa vya kuandikishia wapigakura.
Uandikishaji
katika Mkoa wa Dar es Salaam ulitarajiwa kuanza Julai 4 mwaka huu,
lakini ukasogezwa mbele hadi Julai 16, tarehe ambayo nayo ilisogezwa
mbele ili kutoa fursa kwa wananchi kusherekea Sikukuu ya Eid el Fitr.
0 comments:
Post a Comment