SAFI! Mke wa Rais mama Salma Kikwete ameibuka na kuwa gumzo baada ya kifo cha mwanamuziki nyota, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ kufuatia ahadi yake ya kumsomesha mtoto wa marehemu, Haji ambaye yupo kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Turiani, iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wanamuziki na familia ya marehemu, walisema kitendo cha Mama Salma kimewatia nguvu ya kujua kuwa serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na wasanii kwa jamii, kitu walichotaka kiigwe na wengine.
Kaka wa marehemu Banza aitwaye Hamis, alisema familia inamshukuru sana mama huyo kwa kujitolea kwake kwani ameona thamani ya kazi ya ndugu yao.
“Tunam-shukuru sana Mama Salma kwa uamuzi wake wa kumsaidia huyu mtoto, Mungu atambariki, pia tunawashukuru wote waliokuwa pamoja nasi tangu kumuuguza mpaka kifo chake,” alisema Hamis.
Mwajiri wa zamani wa Banza Stone na mdau mkubwa wa muziki wa dansi nchini, Asha Baraka pia alimpongeza Mama Salma kwa kuonesha moyo wa kuwathamini wasanii wa muziki wa dansi na kwamba serikali inathamini mchango wa wanamuziki wa dansi.
Aidha, kabla ya Mama Salma kuamua kumsomesha mtoto wa Banza, mtoto huyo aliyekata tamaa kwa kutojua angesomaje akizungumza na mwanahabari wetu alinukuliwa akisema: “Kifo cha baba kimeniacha kwenye wakati mgumu sana, sijui maisha yangu kielimu yatakuwaje.”
Hata hivyo, Haji alimemshukuru Mama Salma Kikwete kwa msaada aliompa kielimu.
Kwa upande wake, mnenguaji nyota ambaye amewahi kufanya kazi kwa muda mrefu na marehemu, Super Nyamwela alisema Mama Salma amefanya kitu kizuri kinachoonesha thamani ya wasanii mbele ya serikali na kumpongeza kwa kuchukua jukumu la kumsomesha mtoto huyo.
Mwimbaji mwingine nyota aliyewahi kufanya kazi na marehemu wakiitumikia Bendi ya Extra Bongo, Rama Pentagon naye alimpongeza Mama Salma kwa uamuzi wa kumsomesha Haji.
0 comments:
Post a Comment