
Watoto hao ambao wamefahamika kwa majina ya Agustino Steven (8) na Rebeka Steven(7) ni wanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Mapambano iliyopo Kata ya Iyela Jijini Mbeya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti , watoto hao wamesema Wazazi wao waliwaacha kwenye nyumba ya kupanga tangu mwezi wa Mei mwaka huu ambapo Baba inasadikika alielekea Umalila Mbeya Vijijini ambako inasemekana ameoa mke mwingine.
Wamesema Mama yao alielekea Mbozi ambako pia naye inasadikika ameolewa na mwanaume mwingine hivyo kuwaacha watoto bila kuwa na huduma za msingi kama Chakula na mavazi huku wakiwa wameachiwa nyumba mtaa wa Jakaranda Airport.
Watoto hao waligundulika baada ya kukutwa mitaani wakitafuta riziki kwa kuzoa taka kwenye majumba ya watu kisha kupeleka majalalani kwa ujira wa kati ya shilingi 200 na 500 ambazo huzitumia kununua mahitaji ya nyumbani pamoja na kujipikia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia chini ya Jeshi la Polisi, Mary Gumbo amesema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kuwahoji watoto hao ambapo pia aliwaomba majirani na wananchi kulisaidia jeshi la Polisi ili kuwabaini wazazi walipo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Amesema majirani pia waendelee kuwa karibu na watoto hao hadi pale wazazi wao watakapopatikana kwa kuwahudumia na kuhakikisha wanaendelea na masomo kama kawaida.
Gumbo amesema kitendo kilichofanywa na wazazi hao ni cha kinyama hivyo wakipatikana hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ambapo pia alitoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya kikatili.






0 comments:
Post a Comment