
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewachokoza tena wabunge baada ya kuitaka Serikali kuanza kukata kodi katika posho za wawakilishi hao ili kuongeza wigo wa mapato.
Zitto
amesema hatua ya Serikali kuondoa msamaha wa kodi katika malipo ya
kiinua mgongo cha wabunge katika bajeti ya Serikali ya 2016/17 ni jambo
jema lakini isiishie hapo kwa kuwa viongozi hao bado wana mapato mengi
yasiyokatwa kodi yakiwemo ya posho.
Kauli
ya mbunge huyo wa Kigoma Mjini ni mwendelezo wa msimamo wake wa kupinga
wabunge kulipwa posho ya vikao bungeni na katika Bunge la 10 alipokuwa
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) aliongoza kampeni ya kupinga
ongezeko la posho hiyo bila mafanikio.
Aidha,
pendekezo lake kutaka posho za wabunge zikatwe kodi limekuja siku mbili
tangu Naibu Spika, Dk Tulia Ackson atangaze kukata posho za wabunge
watakaokuwa wakisaini kuingia bungeni na baadaye kuondoka na waathirika
wa kwanza wa hatua hiyo watakuwa wapinzani wanaosusia vikao vyake.
Akitoa
maoni katika mchaparo wa uchambuzi wa Bajeti ya Serikali ya mwaka
2016/17 ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya KPMG juzi usiku,
Zitto alisema kiinua mgongo hicho kilichoanza kutolewa mwaka 2010
kimekuwa kikitolewa bila kufuata sheria.
Alisema
mwaka 2010 pensheni hiyo iliongezwa mara mbili kinyume na sheria na
mwaka jana fedha hizo ziliongezwa tena takriban mara nne zaidi bila
kukatwa kodi.
Zitto alisema wanashangaa kwa nini kodi ya kiinua mgongo imeanzishwa mwaka huu wakati wabunge watalipwa mwaka 2020.
“Nilichokuwa
na natarajia ni kuanzisha kodi kwenye posho. Sisi (wabunge) tuna posho
za aina nyingi na kubwa zaidi ni ile posho ya kikao ya Sh220,000 kwa
siku,” alisema.
“Hii posho haikatwi kodi na wala siyo fedha za kujikimu (per diem) ambayo unapewa kwa ajili ya chakula na malazi.”
Alisema
kwa mwaka mbunge anapata takriban Sh40 milioni za posho (Sh200 milioni
kwa miaka mitano) wakati kiinua mgongo ni takriban Sh172 milioni baada
ya miaka mitano hivyo posho zingeweza kuingiza mapato mengi zaidi.
Katika
uchambuzi wa bajeti hiyo, Mkurugenzi wa kodi na huduma wa kampuni wa
KPMG, David Gachewa alisema uanzishwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) katika sekta ya benki utawaumiza wananchi lakini hakukuwa na namna
nyingine zaidi ya Serikali kuianzisha ili kuongeza wigo wa mapato.
Hata
hivyo, alisema anaona utata katika utekelezaji wa ukusanyaji mapato
hayo iwapo Serikali itatoa mashine za kielektroniki za kutolea risiti
(EFD) kwa benki hizo au Kamishna Mkuu wa TRA atawaandikia barua
kutozitumia mashine hizo kama Serikali ilivyompa madaraka hayo katika
bajeti.
“Hii
siyo mara ya kwanza kuwapo ugumu katika utekelezaji wa baadhi ya hatua
za ukusanyaji mapato. Naamini Chama cha Benki Tanzania (TBA) kitakaa na
Serikali kuona ni namna gani watalitatua tatizo hilo,” alisema Gachewa.
Kuhusu
hatua ya Serikali kuzitaka taasisi zote za umma kutumia huduma za bima
za Shirika la Bima la Taifa (NIC), Gachewa alisema si kitu kizuri kwa
sababu kitafanya Serikali ianze kushindana na sekta binafsi.
“Kuna
dalili za wazi kuwa Serikali inafanya biashara jambo ambalo
halikutarajiwa. Serikali ilitakiwa iache sekta ya bima mikononi mwa
sekta binafsi na yenyewe iweke mazingira wezeshi,” alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo alisema
hatua nyingi zilizochukuliwa katika uandaaji wa bajeti hizo zimekosa
ushahidi kama zitatekelezeka ipasavyo.
Mtaalamu
huyo wa masuala ya elimu na saikolojia alisema uamuzi wa kupunguza
safari za nje una matatizo sababu unaifanya Tanzania kutokuwa na
muunganiko na ulimwengu na kitendo cha bajeti hii kubana zaidi matumizi
kitaifanya nchi ishushe hadhi yake kimataifa.
“Jambo
la msingi katika udhibiti wa safari za nje lingekuwa kupunguza posho za
maofisa wanaosafiri nje ya nchi na siyo kupiga marufuku mpaka kwa
kibali maalum,” alisema.
Kuhusu
bajeti ya elimu, Profesa Kitila alisema iwapo fedha zote Sh4.4 trilioni
zilizopangwa zitatolewa ni jambo jema katika sekta hiyo muhimu katika
maendeleo.
Hata
hivyo, alionya kuwa historia inaonyesha bado hazitaleta matokeo mazuri
kwa kuwa sehemu kubwa huelekezwa katika kulipa mishahara na kuimarisha
miundombinu badala ya kugharamia programu za kuongeza ubora wa taaluma.
Wadau
wengi waliipongeza Serikali kutenga asilimia 40 ya bajeti katika miradi
ya maendeleo ila walionyesha hofu kuwa sehemu kubwa ya kodi inategemea
sekta binafsi jambo linaloweka ugumu katika mazingira ya ufanyaji
biashara.
Profesa
wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema takriban
asilimia 51 ya mapato ya bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Phillip Mpango inagusa sekta binafsi na kuhoji kama
kutakuwa na ukuaji mzuri wa sekta hiyo.
“Uamuzi
wa kuanzisha VAT katika utalii haukuwa mzuri badala yake Serikali
ilitakiwa ivutie watalii wengi ili ipate kodi katika maeneo mengine ya
tozo kutokana na idadi kubwa,” alisema na kuongeza: “Kodi inatakiwa kuwa chombo cha mapato na msingi mkubwa wa maendeleo.”
0 comments:
Post a Comment