Wakati
aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitengua uamuzi
wake wa kung’atuka kwenye wadhifa huo na kuomba kurejea, viongozi wa juu
wa chama hicho wamepinga hatua hiyo wakisema katiba yao hairuhusu na
kwamba anakwenda kukiua chama.
Kauli
za viongozi hao, zimekuja muda mfupi baada ya Profesa Lipumba kutangaza
nia hiyo jana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni huku
akibainisha kuwa amefanya hivyo baada ya kuombwa.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba hawezi
kuwa na nia njema ya kukijenga chama hicho endapo atarudishwa kwenye
nafasi aliyoikataa.
“Anataka kuja kukiharibu chama,”
alisema Mazrui. Alifafanua kuwa tayari chama hicho kimefanya mambo
mengi bila Lipumba ambaye alikuwa anaona kila kinachoendelea, hivyo
alichokisema hakina mashiko kwani CUF ilisharidhia kuitisha mkutano wa
uchaguzi kujaza hiyo.
Akieleza sababu alizozitoa mwenyekiti huyo, Mazrui alisema haoni chochote cha maana. “Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni nini?” alihoji naibu katibu mkuu huyo.
Alisisitiza
kuwa Wazanzibari wanaendelea na mchakato wa kuidai haki yao iliyoporwa
Oktoba 25 na hawana nafasi ya kushughulika na masuala yasiyokuwa na tija
kwao, hivyo haoni kama kuna sababu ya kumjadili Lipumba na nafasi yake
badala ya kuendelea pale walipo.
“CCM
wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja kuharibu
mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili.Tunataka haki iliyoporwa,” alisisitiza.
Msimamo
wa Mazrui haukutofautiana sana na ule wa Kaimu Mwenyekiti wa chama
hicho, Twaha Taslima aliyebainisha kuwa amesikia taarifa za kurudi kwa
Profesa Lipumba, lakini haoni uwezekano huo.
“Katiba
hairuhusu hilo.Hakuna kifungu kinachotoa nafasi kwa kiongozi
aliyejiuzulu kurudi kwenye nafasi yake pindi atakapotaka kufanya hivyo,” alisema Taslima.
Aliielezea
Ibara ya 117 (2) iliyotumiwa na Profesa huyo kuandika barua ya kutengua
uamuzi wake, kuwa inatoa tafsiri zaidi ya moja hivyo kuwapo haja ya
viongozi kukutana na kujadili suala hilo kabla ya kutoa maamuzi.
Kwa kuwa hakuwapo kwenye mkutano huo, Taslima alisema: “Tunahitaji kukutana haraka na kujadili. Tutafanya mkutano wetu na tutavijulisha vyombo vya habari ndani ya wiki hii.”
Taslima
alisema kipindi alichoongoza kilikuwa na changamoto nyingi ambazo ni
tofauti na sasa, hivyo haoni haja ya mtu mwingine kuja wakati mambo
yametulia. Chama hicho kilipanga kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo
Agosti mwaka huu.
Baada
ya kung’atuka kwa Lipumba, Taslima alichukua mikoba yake na kukivusha
chama hicho kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, pamoja na ule
wa Zanzibar ambao uliahirishwa na chama hicho kususia marudio yake
Machi 20 mwaka huu.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya alisema
upo uwezekano wa Lipumba kurudi kwenye nafasi yake kwasababu mpaka sasa
haijazibwa.
“Mwenyekiti
huchaguliwa au kutenguliwa na halmashauri kuu. Haikupitisha kujizulu.
Barua ya kujiuzulu itaenda pamoja na hii ya kutengua uamuzi wa awali,” alisema Kambaya.
Kauli ya Lipumba
Awali,
Profesa Lipumba alisema mara kadhaa amekutana na viongozi wa dini na
chama pamoja na wanachama wa CUF na wote walikuwa na ujumbe mmoja
tu…’rudi tukijenge chama.’
Profesa
Lipumba hakushiriki mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana
ambao kwa upande wa Zanzibar, kutokana na hitilafu zilizojitokeza
ulifutwa na kurejewa Machi 20 mwaka huu huku chama hicho kikiwa
kimesusia marudio hayo.
Pamoja
na hayo yote, Lipumba alisema ametafakari sana juu ya hali ya kisiasa
Zanzibar na kuona umuhimu wa kutoa ushirikiano ili mambo yaende kwa
manufaa ya taifa.
“Ni
lazima nchi iendeshwe kwa misingi ya demokrasia ambayo itapatikana kwa
umoja wetu.Nimerudi kushirikiana na wenzangu kutimiza malengo hayo ili
kuchangia maendeleo ya Tanzania,” alisema Profesa Lipumba.
Lipumba
aliachana na uongozi wa chama hicho, Agosti 8, mwaka jana, siku chache
baada ya vyama vinavyounda Ukawa kukubaliana kumsimamisha Edward
Lowassa.
Alimuandikia
barua Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad kuwa hakubaliani na
uamuzi wa chama chake kuridhia makada waliohama Chama cha Mapinduzi
(CCM), akiwemo Lowassa, kupewa fursa ya kugombea nafasi za uongozi.
Baada
ya kukatwa kwenye mchujo wa ndani ya CCM, Lowassa akiwa na makada
kadhaa wa chama hicho akiwamo aliyewahi kuwa waziri mkuu, Frederick
Sumaye, alihamia Chadema ambako alipewa fursa ya kupeperusha bendera ya
chama hicho kilichomo ndani ya Ukawa.
Lipumba hakukubaliana na hilo, alikaa pembeni na kuachia ngazi ingawa alishiriki tukio la kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa.
Jana,
wakati anatangaza kufanya mabadiliko ya kile alichokiamua miezi 10
iliyopita, hakuruhusu maswali, ila alifafanua kile kitakachofuata baada
ya kuwasilisha ombi hilo, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho: “Katibu Mkuu anashauriana na wanasheria kabla suala langu halijapelekwa kwenye halmashauri kuu kama katiba inavyosema,” alisema Profesa Lipumba.
0 comments:
Post a Comment