Friday, May 6, 2016

Walimu Wagoma, Kisa Mwenzao Kuzabwa Kofi Darasani na Ofisa Elimu

WALIMU wa shule ya msingi Kianda wameanza mgomo wa siku mbili wa kutofundisha shuleni hapo huku wakilaani kitendo cha Ofisa Elimu (Shule za Msingi) wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Peter Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao akiwa darasani mbele ya wanafunzi wake.

Makamu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Flora Kipesha alisema wameitisha mgomo huo wa siku mbili kupinga kitendo cha Fusi kumshambulia na kumpiga makofi mwalimu mwenzao Jacob Msengezi (25) ambaye anafundisha somo la Hisabati Darasa la Saba shuleni hapo.

“Licha ya kulaani vikali kitendo hiki cha udhalilishaji alichofanyiwa mwalimu mwenzetu na Ofisa Elimu (DEO) wetu (Peter Fusi) kumcharaza makofi mbele ya wanafunzi wake akiwa darasani ….Ametudhalilisha sote yaani hata hamasa ya kufundisha imetoweka ….. 

“Sasa hatutaingia darasani kufundisha kwa siku mbili tukimshinikiza Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga (Adam Missana) achukue hatua dhidi ya ofisa huyo wa elimu ……yaani tunadhalilishwa hivi mbele ya wanafunzi wetu wenyewe wakati kazi hii tumeisomea na tuna vyeti halali ….Tukiwa na sifa stahiki za taaluma ya ualimu,” alieleza Kipesha. 

Akifafanua, alisema walimu hawataingia kufundisha kwa siku hizo mbili na watakuwa ofisini wakiandaa mitihani huku wanafunzi wakiendelea kuhudhuria shuleni hapo kama kawaida.

Mwalimu Msengezi alisema tukio hilo lilitokea Jumatano saa tatu asubuhi shuleni hapo baada ya ofisa elimu huyo kufanya ziara ya kikazi.

“Nilikuwa na kipindi cha somo la hesabu kuanzia saa mbili hadi saa 2.40 asubuhi kwa kuwa mwalimu wa somo la Kiingereza alikuwa ‘busy’ niliamua kubakia darasani humo nikisahihisha madaftari ya wanafunzi wangu, ndipo nikamwona akiwa eneo la shule, hivyo nikaamua kwenda ofisini kujiandaa na ukaguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Wakati nikiwa ofisini aliingia chumba cha darasa la saba na kukuta wanafunzi wakiwa pekee yao, ndipo alipoamuru aitwe mwalimu aliyekuwa akifundisha darasa hilo.

“Nilikwenda darasani na kukutana naye, nilimweleza ilivyokuwa, basi akaniuliza kwani sasa ni saa ngapi?

"Nilipomjibu kuwa ni saa tatu asubuhi alighadhabika na kunipiga makofi. Nilipohisi anajiandaa kuniadhibu zaidi nilitimua mbio na kutoka darasani,”
alisema mwalimu huyo.

Aliongeza kuwa tayari ameshafikisha malalamiko yake kwa Katibu wa Chama cha Walimu nchini (CWT) Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Vicent Ndewele kwa hatua zaidi.

Ndewele amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akiahidi kuwa chama hicho kitatoa msimamo wake kwa vyombo vya habari.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger