Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Pwani limemkamata mmoja wa
wamiliki wa eneo la maegesho ya magari la White Star, Munira Mbowe
akidaiwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.
Mbowe ambaye
ni mmiliki wa eneo hilo lililopo Kiluvya kwa Komba nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam, alikamatwa jana baada ya kufanyika msako wa kushtukiza
kwa watu wanaodaiwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.
Inadaiwa kuwa Mbowe amelisababishia shirika hilo hasara ya Sh50 milioni.
Akizungumza
kwenye eneo hilo, Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Pwani, Henry
Byarugaba alidai kuwa baada ya kufanya ukaguzi waligundua umeme uliokuwa
ukitumika katika eneo hilo haukuunganishwa na Tanesco.
“Tumekuwa
tukibuni mbinu mpya kila kukicha ya kuwatia mbaroni wateja wetu
wanaotuhujumu na leo (jana), tumembana huyu anayedaiwa ni mmiliki wa
yard hii ya White Star baada ya kukuta anatumia umeme wa wizi
uliounganishwa katika njia tatu,” alidai Byarugaba.
Alisema tayari wameshamfikisha Kituo cha Polisi Kibaha na hatua zingine za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.
Hata
hivyo, alidai kuwa hiyo siyo mara ya kwanza kwa Mbowe kukamatwa kwa
kosa hilo. Alidai mwaka jana Tanesco ilipofanya msako, ilimkamata akiwa
amejiunganishia umeme na alichukuliwa hatua za kisheria.
Alipoulizwa kama tuhuma hizo zina ukweli, Mbowe alijitetea kuwa
hajui ni nani aliyemuunganishia njia hizo tatu za umeme kwa sababu mara
nyingi hufanya shughuli zake jijini Dar es Salaam, mara chache hufika
kwenye yard hiyo kufanya kazi zingine ambazo ni chache.
“Ni
kweli tumekutwa na kosa la kuiba umeme, lakini jamani nataka niwaeleze
kuwa mimi sihusiki na kingine, nawaomba msinitoe kwenye vyombo vya
habari, haya ni maisha tu, sio vizuri kunitoa jamani mimi sihusiki
kabisa katika wizi huu,” alijitetea Mbowe.
Kaimu Meneja wa
Taneso Mkoa wa Pwani, Selemani Mgwila alisema kitendo alichokifanya
mteja wao huyo ni kosa kwani umeme waliokuwa wanautumia umesababisha
upotevu wa mapato makubwa ya shirika.
“Tunalalamika kila siku
mpaka shirika linaonekana halifanyi kazi kwa sababu ya hawa watu
wachache, safari hii lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment