Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na
tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja waliokatwakatwa mapanga
baada ya kuvamiwa nyumbani, katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema,
mkoani Mwanza, siku ya Jumatano usiku.
Wizara
inalaani vikali mazingira ya mauaji ya watu hao wa familia moja, ambapo
wauaji walivamia nyumba ya mama mjane na kumuuwa yeye mwenyewe, na watu
wengine sita wakiwemo watoto watatu.
Wizara
inapongeza utayari wa uongozi wa mkoa wa Mwanza na jeshi la Polisi
amabo waliweza kufika sehemu ya tukio ili kufuatilia mauaji hayo. Ni
imani ya Wizara kuwa Polisi kwa ushirikiano wa wananchi wa wilaya ya
Sengerama wataweza kuwasaka watuhumiwa wa mauaji na kuwachukulia hatua
kali.
Wizara
inawasisitiza wananchi kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwamata
watuhumiwa ili kuondoa hofu miongoni mwa familia za kijiji cha Sima na
wilaya ya Sengerema. Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutarejesha imani na
utulivu miongoni mwa wakazi wa Sengerema na hivyo kuweza kuendelea na
shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Wizara
inasisitiza kwamba kila binadamu anayo haki ya kuishi na kupata
hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa Sheria za nchi. Vitendo vya mauaji
ya kikatili vinapotokea katika familia zetu vinasababisha hofu kubwa
miongoni mwa wanafamilia. Mauaji hayo yanawakosesha amani wanafamilia na
yanadhohofisha ari ya ndugu wa familia kufanya shughuli zao kwa
amani.
Wizara
inaomba wanafamilia waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa subira katika
kipindi hiki cha majonzi makubwa, wakati Serikali ikiendelea na
jitihada za kuwasaka watuhumiwa wa mauaji hayo.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
12/5/2016
0 comments:
Post a Comment