Wakati
viongozi wakiendeleza kasi ya Rais John Magufuli ya utumbuaji wa
majipu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wanaoiga
kasi hiyo kutenda haki, ikiwamo kufuata taratibu na sheria.
Akizungumza
kwenye maadhimisho Siku ya Wauguzi Duniani mkoani Geita jana, Samia
aliwataka viongozi na wanasiasa kufuata taratibu za kazi, ikiwamo kutoa
nafasi ya kujitetea kwa watumishi wanaotuhumiwa.
Alitoa kauli hiyo, baada ya wauguzi kulalamika kwenye hotuba yao kwamba kuna viongozi waliwatumbua wauguzi bila kuwatendea haki.
“Hata
hivyo, nakiomba Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), kuweka utaratibu wa
kufuatilia maadili ya wauguzi na kuwachukulia hatua za kisheria, wale
wote ambao wanakwenda kinyume na kiapo chao cha kazi,” alisema.
Rais
wa Tanna, Magesa Paul alimuomba Makamu wa Rais kutembelea maeneo yao ya
kazi, ili ajionee hali halisi ya wauguzi wanavyofanyakazi katika
mazingira magumu, ikiwamo kukosa vitendea kazi na nyumba za kuishi.
Jijini
Dar es Salaam, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa, Paul
Makonda aliwataka wauguzi kuhakikisha wanatii maadili ya kazi, bila hofu
ya kupigiwa simu na baadhi ya viongozi wa Serikali waliozoea kutaka
upendeleo wa huduma, kinyume na maadili yao.
“Tunaomba
wauguzi mkitendee haki kiapo chenu cha kazi, na mtumie siku hii muhimu
kuutathmini utendaji wenu wa kazi katika kuwasaidia wananchi,” alisema.
Alisema
Serikali inatambua changamoto za wauguzi, hivyo wasitumie matatizo yao
katika kuwanyanyasa wagonjwa, bali wawasaidie na kuwaonyesha upendo.
Akisoma
risala kwa niaba ya wauguzi wenzake, muuguzi wa Hospitali ya Temeke,
John Mgonja alilaani tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kutumia
madaraka kuvuruga utaratibu wa muda wa kuwaona wagonjwa.
“Bila
kujali muda uliowekwa wa kuwaona wagonjwa, baadhi ya viongozi hutaka
kuingia kuwaona wagonjwa wao kutokana na madaraka waliyo nayo, bila
kujali kuwa kufanya hivyo kunachelewesha huduma,” alisema.
Mganga
Mkuu wa Mkoa, Musa Wambura aliwaomba wauguzi kuhakikisha wanafanya kazi
kwa umakini na weledi, ili kuepusha lawama kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment