MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imemwachia huru Justine Kasusura na
kumfutia adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 35 kwa kosa la wizi na
unyang’anyi wa dola za Marekani milioni mbili (karibu Sh bilioni 4.4 kwa
viwango vya sasa vya kubadili fedha)kwa kutumia silaha.
Kasusura alikaa gerezani miaka 15, ambayo tisa kati yake alitumikia
kifungo na sita alikuwa rumande kwa sababu ya kukosa dhamana wakati wa
usikilizwaji wa kesi.
Aliachiwa huru juzi na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa;
Jaji Mbarouk Mbarouk, Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles Kaijage.
HUKUMU JOPO LA MAJAJI
Hukumu ya jopo la majaji hao iliyotolewa Mei 9, mwaka huu, imesema
Mahakama ya Rufaa haiwezi kukubaliana na upande wa Jamhuri kwamba
vitendo vya mkata rufaa (Kasusura) vya kukimbia kimbia mikoani baada ya
tukio la ujambazi, vingesababisha kuamini kuwa lazima alishiriki kutenda
kosa hilo lililomtia hatiani.
“Kutokana na upungufu huo na mwingine, imeifanya mahakama kuamini
kwamba kesi dhidi ya Kasusura haikuthibitishwa bila kuacha shaka.
“Tumeikubali sababu ya tatu ya rufaa iliyowasilishwa na mrufani
kwamba ni ya msingi, hivyo tumeikubali rufaa yake, tunafuta kutiwa
hatiani kwa mrufani pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka 35 jela,”
lilisema jopo na kuamuru Kasusura aachiwe huru mara moja.
Hukumu hiyo inasema hati ya mashtaka ilionyesha kwamba dola milioni
mbili zilizoibwa zilikuwa mali ya Citibank, lakini hakuna ushahidi
ulioonyesha kuthibitisha kilichosemwa katika hati ya mashtaka.
“Ushahidi ulishindwa kuweka bayana nani alikuwa mmiliki wa fedha hizo zilizoibwa hivyo kuacha mashaka yanayompa faida mrufani.
“Tunakubaliana na mrufani kitendo cha kushindwa kumwita mahakamani
ofisa kutoka Citibank ambaye ni mmiliki wa fedha hizo inaleta shaka
kuamini kwamba kiasi hicho cha fedha kinachodaiwa kuibwa ndicho
kilichoingia, hiyo ilisemwa awali kwamba vielelezo havisapoti kiasi cha
fedha kilichokuwa katika hati ya mashtaka,” inasema hukumu hiyo.
KIINI CHA KESI
Kasusura na wenzake sita walishtakiwa kwa mara ya kwanza katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka 2001 wakikabiliwa na mashtaka
matano.
Walishtakiwa kwa kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi na mashtaka mawili ya kupokea mali inayosadikiwa kuwa ya wizi.
Kasusura aliyekuwa dereva wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support,
alitumwa na meneja wa kampuni hiyo akiwa na mwenzake Said Mussa kuchukua
mzigo wa fedha Uwanja wa Ndege wa Juliuis Nyerere kuupeleka Citibank.
Mussa katika ushahidi wake alidai walipotoka Uwanja wa Ndege, hatua
chache walikuta gari imeegeshwa na Kasusura akaenda kuegesha gari lenye
mzigo wa fedha mbele ya gari hilo.
Alidai Kasusura alimwambia kwamba mchezo umeishia hapo, akamshikia
bastola akimtaka kufungua boksi lililokuwa na fedha, akachukua funguo na
kulifungua, mara aliona watu asiowafahamu wakivamia na kuondoka na
fedha.
Baada ya tukio hilo, Kasusura alikimbilia mikoa mbalimbali, ikidaiwa
kila alipokuwa akipita alikuwa akiwapa rushwa askari na wengine
walituhumiwa kumsindikiza hadi mkoani Mbeya.
Hata hivyo waliposhtakiwa
kwa rushwa waliachiwa huru kwakuwa upande wa mashtaka ulishindwa
kuthibitisha mashtaka dhidi ya polisi hao.
Kasusura alikaa mkoani Mbeya hadi Desemba 24, 2001 alipokamatwa akiwa
katika nyumba ya wageni ya Moon Dust na alikana kwenda Tanga, Arusha na
Sumbawanga na kueleza kwamba alipitishwa maeneo hayo na polisi.
Upande wa Jamhuri ulipofunga ushahidi wake, washtakiwa wengine
waliachiwa baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu.
Mwisho wa kesi
iliposomwa hukumu mwaka 2007 na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa
Mahakama ya Kisutu ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Sivangilwa
Mwangesi, Kasusura alitiwa hatiani baada ya mahakama kujiridhisha kwa
ushahidi uliotolewa kwamba alitenda kosa.
Kasusura alihukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la wizi, miaka 30 na fimbo 12 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
MKEWE AFARIKI DUNIA
Siku chache baada ya hukumu hiyo, Kasusura alimpoteza mkewe ambaye alifariki dunia.
Kasusura hakuweza kupata ruhusa ya kwenda kumzika mkewe, aliyeacha
mtoto wa kike ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kati ya tisa na
10.
Mtoto huyo alikuwa akifika mahakamani na mama yake kila kesi
ilipokuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam.
RUFAA
Baada ya kutiwa hatiani, Kasusura alikata rufaa Mahakama Kuu mwaka 2007.
Kasusura alishindwa Mahakama Kuu, lakini alikata rufaa Mahakama ya
Rufaa Juni 23, 2010 akitoa sababu nane za kupinga kutiwa hatiani na
adhabu aliyopewa.
Miongoni mwa sababu hizo alidai Jaji wa Mahakama Kuu alijielekeza
vibaya kukubaliana na hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na
kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha
shaka.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini
Kweka ulijibu kwa kwamba upande huo uliweza kuthibitisha mashtaka dhidi
ya mrufani bila kuacha shaka yoyote.
Kweka alikubali kwamba mshtakiwa alikamatwa Desemba 24, 2001 lakini maelezo yake yalichukuliwa Desemba 26, 2001.
Alidai katika maelezo haikuonyesha kwamba kulikuwa na maombi ya
kuongeza muda wa kuchukua maelezo hayo na mshtakiwa aliyakana, lakini
hapakuwepo na kesi ndani ya kesi kuthibitisha maelezo hayo aliyokana
yalikuwa ya kwake.
Ilidaiwa mbali na ushahidi huo wa maelezo, lakini kuna ushahidi wa
mashahidi wengine uliweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
MAGEREZA
MTANZANIA ilipata nafasi ya kuzungumza na Ofisa Magereza wa Gereza la
Ukonga (Jina tunalo, si msemaji) ambako Kasusura alikuwa alikuwa
akitumiakia adhabu yake tangu alipohukumiwa kifungo mwaka 2007.
Ofisa huyo alisema Kasusura baada ya kumaliza utetezi katika Mahakama
ya Rufaa, majaji waliandika hukumu na Jumatatu wiki hii iliandikwa hati
ya kumwita mahakamani.
Jumanne Kasusura alipanda gari la Magereza asubuhi akiwa kavalia
suti, kwenda mahakamani na ndipo alipoachiwa na kuchukuliwa na ndugu
zake.
GEREZANI
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu maisha ya Kasusura alipokuwa
gerezani, ofisa huyo alisema: “Katika kipindi chote alichokaa gerezani
alikuwa mtiifu sana, mnyenyekevu, mwenye nidhamu na alikuwa mshauri
mzuri wa wafungwa wengine.
“Alikuwa mnyapara (kiongozi wa wafungwa wenzake), alikuwa ni mfungwa wa mfano, alionyesha wazi kwamba alikuwa karekebishika.
“Akiwa gerezani hajawahi kufanya tukio baya la aina yoyote. Alikuwa
hajui kushona, lakini alijifunza kushona akiwa gerezani na alifikia
hatua ya kushona hadi nguo za wafungwa.”
0 comments:
Post a Comment