Serikali
imesema imeshtushwa na wimbi kubwa la vijana wa Kitanzania wanaojiunga
na makundi hatari ya kigaidi ya Al-Shabaab na Islamic State, maarufu
kama ISIS.
Kauli
hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi wakati akiwasilisha bajeti ya
wizara yake ya Sh trilioni 1.6 kwa mwaka 2016/17.
Dk.
Mwinyi alisema pamoja na hali hiyo, Serikali imeendelea kupambana na
makundi hayo kwa kila njia ili kuhakikisha nchi inakuwa salama katika
maeneo yote, yakiwamo ya mipakani.
Alisema matukio ya kigaidi yameendelea kuwa tishio duniani, hivyo Tanzania inapaswa kuchukua tahadhari ya kila namna.
Dk.
Mwinyi alisema kuwapo kwa makundi hayo ya Al-Shabaab, Al-Qaeda, Boko
Haram na Islamic State, kunafanya tishio la ugaidi kusambaa duniani
kote.
“Taarifa
za kuwapo baadhi ya Watanzania wanaojiunga na makundi ya Al-Shabaab na
ISIS tunazo, kunahatarisha usalama wa Tanzania, hasa ikizingatiwa
kiujumla mwingiliano mkubwa uliopo kati ya wananchi wetu na watu wenye
malengo tofauti.
“Hatari
iliyopo ni uwezekano wa baadhi ya vijana waliojiunga na makundi ya
kigaidi ya kimataifa kurejea nyumbani kwa lengo la kutekeleza vitendo
vya kigaidi nchini mwetu.
“Tuna kila sababu ya kujizatiti na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema
kipindi kilichopita, kumejitokeza viashiria vyenye mwelekeo wa kigaidi,
ikiwemo kuvamiwa baadhi ya vituo vya polisi, kuporwa silaha na baadhi
ya askari kuuawa na kundi ambalo nia yake haijafahamika.
“Matukio
yenye mwelekeo wa kigaidi, ni kama yaliyotokea katika mapango ya Amboni
mkoani Tanga, Kitongoji cha Nyandeo wilayani Kilombero pale Morogoro na
kukamatwa mabomu ya kutengenezwa kwa mkono katika maeneo mbalimbali
yakiwamo Zanzibar,” alisema.
Alisema
pamoja na hali hiyo, kwa upande wa mpaka wa kusini mwa nchi, hali
imeendelea kuwa shwari, licha ya uwapo wa utata wa mpaka wa Ziwa Nyasa
ambao bado haujapatiwa suluhisho.
Kutokana
na hali hiyo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kwa
kutoa taarifa ya matukio yanayotishia kuashiria uvunjifu wa usalama.
Kuhusu
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na ule wa marudio
uliofanyika Machi 20, mwaka huu Zanzibar, alisema umefanyika kwa amani
na utulivu, licha ya baadhi ya maadui wa ndani na nje kutabiri mambo
mabaya.
“Watanzania
tunayo sababu ya kujivunia kuwa uchaguzi mkuu ambao kikalenda ni wa
tano tangu kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uliendeshwa na
kuhitimishwa kwa amani, utulivu na mshikamano mkubwa kinyume na maadui
wetu wa ndani na nje ya nchi waliotutabiria mabaya,” alisema.
Dk.
Mwinyi alisema kwa kutambua umuhimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) kwa vijana, Serikali itaendelea na azma yake ya kuwajenga
vijana uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa na kutoa stadi za kazi.
Alisema
kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, suala hilo sasa litatekelezwa kwa
kutoa mafunzo kwa baadhi ya vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria.
“Katika
mwaka 2015/16, vijana 27,463 walipatiwa mafunzo mbalimbali, yakiwamo ya
kuwapa ujuzi na stadi kazi ili wajiandalie mazingira mazuri ya
kujiajiri.
“Nachukua
fursa hii kuwaomba vijana wanaopata mafunzo ya JKT, wazingatie maarifa
na ujuzi wanaoupata, hususan wa stadi za kazi ili waweze kujiajiri
badala ya imani iliyoanza kujitokeza kwa baadhi ya wahitimu kudai ajira
kwa maandamano.
“Katika
hatua ya kutekeleza agizo la Serikali linalohusu vyombo vyote vya
ulinzi na usalama kuajiri idadi kubwa ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya
JKT, hadi kufikia Februari, mwaka huu vijana 5,453 waliajiriwa na vyombo
vya ulinzi.
“Kati
ya vijana hao, 3,521 waliajiriwa na JWTZ, polisi 1,185, Usalama wa
Taifa 106, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) 617. Hata
hivyo, idadi ya vijana waliopatiwa ajira imeongezeka. Hadi kufikia
Aprili, mwaka huu vijana 7,170 wamejiariwa na vyombo hivyo,” alisema Dk. Mwinyi.
Kambi ya upinzani wahoji wanajeshi kupewa ukuu wa mikoa
Akiwasilisha
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, msemaji wa wizara hiyo, Juma
Hamad Omar, alihoji hatua ya Serikali kuwateua maofisa wa vyombo vya
ulinzi kushika nafasi za kisiasa kama wakuu wa mikoa na wilaya.
Omar
ambaye ni Mbunge wa Ole (CUF), alisema Serikali imekuwa na utamaduni wa
kuwateua maofisa wa vyombo vya dola waliopo kazini, na baada ya uteuzi
huo hufanya kazi kwa mujibu wa chama tawala.
“Wakuu
wa wilaya na mikoa wanafungwa na ibara ya 80 (1) (C) ya Katiba ya CCM
ya mwaka 1977 inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika
wilaya husika. Hali kadhalika wakuu wa mikoa wanafungwa na ibara ya 94
(1) (C) inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika mkoa
husika.
“Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali itambue ibara 147 (3) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka kwamba; ‘Itakuwa ni
marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa,
isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara
5 ya Katiba hii’,” alisema Omar.
Akizungumzia
utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo, alisema katika bajeti ya mwaka
2015/16 Serikali imeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango
kilichoidhinishwa na Bunge kwa miradi ya maendeleo.
0 comments:
Post a Comment