Deni la Taifa limeongezeka kwa Sh7.05 trilioni, kutoka
Sh26.49 trilioni Juni 30, 2014, hadi Sh33.54 trilioni sawa na ongezeko
la asilimia 27.
Kwa
mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Profesa Musa Assad, deni la ndani ni Sh7.99 trilioni huku deni la
nje likiwa ni Sh25.55 trilioni.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana bungeni, alisema kiwango hicho cha ongezeko la deni ni kikubwa katika kipindi cha muda mfupi.
“Uchambuzi
wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharimia madeni ya Sh4.6 trilioni
mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo ya ndani ya Serikali
ambayo ni Sh10.8 trilioni,” alisema.
Alisema
gharama hizo zikijumuishwa na gharama nyingine kama mishahara ya
wafanyakazi na malipo ya likizo, Serikali hubaki na kiasi kidogo cha
fedha za kugharimia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii.
Profesa
Assad alipendekeza mambo matatu kama sehemu ya mikakati ya kukabiliana
na ongezeko la deni hilo, ikiwamo Serikali kuongeza jitihada za ndani za
kuhamasisha ukusanyaji mapato ili kujenga wigo mpana wa kulipa madeni.
Pia, alishauri kuwapo kwa mpango mkakati kuhusu fedha, hasa upunguzaji wa gharama na mikopo yenye masharti.
Jambo
la tatu, alishauri Serikali kuwa na uratibu mzuri wa shughuli
zinazohusisha miamala ya fedha za kigeni, akisema hatua hiyo inawezekana
kama kutakuwapo usimamizi thabiti.
0 comments:
Post a Comment