Mtoto Dorine anayedaiwa kuchomwa mikono na shangazi yake.
Ni ukatili ulioje ambao amefanyiwa mtoto Dorine (12), denti wa darasa la nne Shule ya Msingi Makabe, Mbezi jijini Dar.
Dorine anadaiwa kuunguzwa na maji ya
moto yaliyochemshwa kwenye jiko la gesi na walezi wake wa karibu akiwemo
shangazi yake aliyetajwa kwa jina moja la Scola ambaye alitiwa mbaroni
na bibi yake ambaye haikujikana alipo.
Katika
tukio hilo la Septemba 26, mwaka huu, Scola alidaiwa kutekeleza tendo
hilo, chanzo kikielezwa ni upotevu wa shilingi 20,000.
Kwa mujibu wa chanzo makini, Scola alimtaka Dorine aseme amezipeleka wapi fedha hizo, lakini binti huyo alisema hajui chochote.
Ilidaiwa kwamba, katika hali isiyokuwa ya kibinadamu, wakati Dorine akiwa anahojiwa tayari maji ya moto yalikuwa yakichemka.
Ilisemekana kwamba, baada ya kuona Dorine hataki kusema zilipo fedha hizo, Scola akamuamuru aingize mikono ndani ya sufuria lililokuwa jikoni huku maji yakichemka.
Dorine alipokataa, Scola akadaiwa
kumshika kwa nguvu, akisaidiana na mama yake ambaye ni bibi wa Dorine na
kuizamisha kwenye sufuria la maji mikono hiyo na kumsababishia mtoto
huyo majeraha ya kutisha.
Ilisemekana kwamba, baada ya tukio hilo,
familia hiyo ilifanya siri kubwa na kutompeleka hospitalini lakini
baadhi ya majirani walibaini hilo na kusambaza taarifa ndipo familia
hiyo ikampeleka hospitalini kwa siri.
Alipofikishwa katika Hospitali ya Kanisa
Katoliki Luguruni, Mbezi mtoto huyo alilazwa baada ya mahojiano na
wauguzi ambapo aliwaeleza kila kilichotokea.
Hata hivyo, maelezo ya Dorine kwamba
aliunguzwa na shangazi na bibi yake yalipingwa na Scola ambaye alisema
mtoto huyo alikuwa akikimbia akaangukia maji ya moto.
Taarifa alizopata mwanahabari wetu
kwenye hospitali hiyo kupitia muuguzi wa zamu, zilieleza kuwa taarifa
sahihi za tukio hilo ni zile alizozitoa mtoto huyo.
Katika mahojiano na wauguzi, Dorine
ambaye alikuwa amelazwa kwenye Chumba cha Stuff Na. 16 hospitalini hapo,
alifafanua kuwa anaishi kwa shangazi yake baada ya baba yake mzazi
kuachana na mama yake na baba kuoa mwanamke mwingine.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
ulibaini kwamba, Scola alishikiliwa na Jeshi Polisi Kituo cha
Mbezi-Kwayusuf na baadaye aliachiwa kwa dhamana lakini bibi hakukamatwa.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
RPC Camilius Wambura alipoulizwa na gazeti hili juu ya tukio hilo
alikiri kulijua na kwamba alipokea taarifa za aina mbili hivyo
alimwagiza OCD wa Mbezi-Kwayusuf kulifuatilia na kumpa taarifa kamili.
Alisema taarifa moja ilidai, Dorine
aliunguzwa lakini ya pili ilidai aliangukia kwenye sufuria yenye maji ya
moto hivyo uchunguzi unaendelea ili kupata taarifa kamili.
0 comments:
Post a Comment