Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, ametikisa katika Jimbo la Hai na kumshambulia Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe kwamba ni Mbunge mtalii anayeshinda akizurura Ulaya, huku akishindwa kutatua kero za wapiga kura wake.
Akihutubia
jimboni humo katika siku yake ya kwanza ya kampeni mkoani Kilimanjaro
juzi, Dk. Magufuli aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kwamba, walifanya
biashara ya hasara kumchagua Mbowe kuwa Mbunge wao kwani hajali maslahi
ya wananchi wake.
Awali
mgombea huyo wa CCM alipokelewa na umati wa jimbo hilo kwa mabango
yenye ujumbe mbalimbali yanayoelezea kero za maji, barabara, elimu na
afya, ambayo aliagiza yachukuliwe na msafara wake ili atakapoingia Ikulu
azifanyie kazi kero hizo.
Dk.
Magufuli alisema wananchi wa Jimbo la Hai wameteseka kwa muda mrefu kwa
kuwa na Mbunge ambaye kazi yake imekuwa kuzunguka jijini Dar es Salaam
na mataifa ya Ulaya na Marekani, huku jimbo likikabiliwa na matatizo ya
kijamii kama maji, elimu na ukosefu wa huduma za afya.
“Ingawa
nampenda Mbowe, lakini wananchi wa jimbo hili wanapaswa kufanya
mabadiliko kwa kumtosa Mbunge huyo abaki na nafasi yake ya uenyekiti wa
Chadema ili akaimarishe chama hicho na wamchague mbunge wa CCM ambaye
atawasaidia,” alisema.
Kwa
mujibu wa Dk. Magufuli, Mbowe hawezi kushughulikia masuala ya maendeleo
kwa kuwa anakabiliwa na majukumu mengi ya biashara na uenyekiti wa
Taifa wa Chadema.
“Mbowe
ana nipenda na huwa ana nisifia hadharani kwamba mimi ni mchapakazi na
mimi pia nampenda sana lakini kwenye masuala ya maendeleo ya Watanzania
sitaweka urafiki achaneni naye na mumchague Dunstan Mallya wa CCM
awafanyie kazi watu wa Hai.” alisema mgombea huyo wa CCM.
Alisema
hata Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambayo inaongozwa na Chadema
imeshindwa kuondoa kero za wananchi na kuongeza kuwa ingawa wilaya hiyo
ni ya zamani imebaki nyuma kwa miaka mingi kulinganisha na wilaya mpya.
Akiwahutubia
wananchi wa Siha, mkoani hapa jana, Dk. Magufuli alisema
ameshajihakikishia ushindi wa kishindo na kudai wapinzani wanamsindikiza
na kuwataka wananchi wa jimbo hilo wamchague Agrey Mwanri kwa mara
nyingine awe Mbunge wao kutokana na kazi nzuri aliyowafanyia.
Waziri
wa zamani wa Mambo ya Ndani ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM (Nec), Dk. Emmanuel Nchimbi, aliibukia kwenye kampeni za Dk.
Magufuli wilayani Siha na baadaye Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro jana
na kumrushia makombora mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa.
Dk.
Nchimbi ambaye alikuwa swahiba mkubwa wa Lowassa kwenye harakati za
kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais, alidai Lowassa ni dhaifu na
hawezi kuiongoza Tanzania.
Nchimbi
alisema Watanzania wanahitaji Rais aina ya Magufuli ambaye
atawaendesha mchakamchaka wa maendeleo na si wagombea wengine ambao
historia zao zinaonyesha walishindwa kwenye nafasi za juu walizowahi
kushika.
0 comments:
Post a Comment